Umoja wa Mataifa wasema hali ya Gaza ni giza zito
25 Oktoba 2024Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) lilisema siku ya Ijumaa (Oktoba 25) kwamba raia 430,000 wamekimbilia Syria tangu Israel ilipoanza kuishambulia Lebanon mwezi uliopita, lakini mashambulizi ya mpakani yamekuwa yakihatarisha maisha ya wakimbizi hao na ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.
Mapema leo, mashambulizi ya Israel yameuwa watu watatu kwenye mpaka wa Syria na Lebanon wakati wakikimbia mashambulizi nchini Lebanon, kwa mujibu wa msemaji wa UNHCR katika eneo la Mashariki ya Kati, Rula Amin.
Soma zaidi: Israel yauwa 28 Gaza, 3 Lebanon
"Asubuhi ya leo, tulishuhudia mashambulizi zaidi ya Israel kwenye vivuuko viwili vya mpaka wa Lebanon na Syria. Hali hii inazuwia na inayaweka hatarini maisha ya watu wanaokimbia vita Lebanon na kukimbilia Syria. Kama unavyojuwa, Lebanon imezungukwa na bahari, Syria na Israel. Kwa hivyo, kukimbilia Syria ndilo jambo pekee kwa watu hawa kuondoka Lebanon." Alisema Amin.
Hospitali ya Kamal Adwan yavamiwa
Kwa upande wa vita vya Israel kwenye Ukanda wa Gaza, Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa, Volker Turk, alisema siku ya Ijumaa kwamba hali kwenye ukanda huo ni kama "giza totoro."
"Sera na matendo ya serikali ya Israel kaskazini mwa Gaza zinahatarisha kuwaondosha Wapalestina wote kwenye eneo hilo. Tunachokishuhudia kinaweza kulingana na mateso ya kihalifu, ukiwemo uwezekano wa kutendeka uhalifu dhidi ya ubinaadamu." Alisema kwenye taarifa yake.
Soma zaidi: Lebanon yasema shambulizi la Israel limewaua waandishi wa habari watatu
Wizara ya afya ya Gaza imesema mamia ya wagonjwa na wafanyakazi wa huduma ya afya wamewekwa kizuizini kwenye hospitali ya mwisho kabisa inayofanya kazi katika eneo hilo la kaskazini mwa Gaza.
Wizara hiyo imesema vikosi vya jeshi la Israel vimeivamia hospitali ya Kamal Adwan katika mji wa Jabalia na kwamba bado wanaishikilia hadi sasa, ndani yake wakiwamo pia raia waliojihifadhi kukimbia mashambulizi ya mabomu ya Israel kwenye maeneo ya karibu na hapo.
Wafanyakazi wa afya wagoma kuwaacha wagonjwa
Wafanyakazi wa huduma za afya kwenye hospitali hiyo awali walikataa amri ya jeshi la Israel la kuwataka waondoke na kuwaacha wagonjwa wakiwa hawana wa kuwaangalia.
Kwa upande wake, jeshi la Israel lilidai kuwa operesheni yake kwneye hospitali hiyo inatokana na taarifa za kijasusi kwamba kuna wale iliowaita magaidi na miundombinu ya kigaidi, madai ambayo huyatowa kila linaposhambulia majengo ya umma, kama vile hospitali, skuli, au vituo vya Umoja wa Mataifa.
Soma zaidi: Wajumbe wa Qatar waanzisha tena mazungumzo kuhusu Gaza
Jeshi la Israel lilisema limelazimika kurejea tena kwenye eneo la kaskazini baada ya wanamgambo wa Hamas kujikusanya upya. Jeshi hilo limepoteza wanajeshi wake watatu kwenye mapigano ya hapo jana na Hamas.