Umoja wa Mataifa waunga mkono vikwazo dhidi ya Myanmar
1 Novemba 2023Mjumbe wa Umoja wa Mataifa aliyeteuliwa kuwa mtaalamu wa haki za binaadamu, ambaye ni mpinzani wa serikali ya kijeshi ya Myanmar, ameunga mkono vikwazo vilivyowekwa hivi karibuni na Marekani, Uingereza na Canada kwa makampuni yanayotoa msaada wa kifedha kwa utawala wa kijeshi na maafisa wakuu katika serikali hiyo.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kuongezeka vurugu na ukiukwaji wa haki za binaadamu katika taifa hilo la kusini mashariki mwa Asia.
Hapo jana wizara ya mambo ya nje ya Marekani, ilisema inaiwekea vikwazo kampuni ya serikali ya mafuta na gesi ambayo ndio inayochangia pakubwa pato la taifa. Maafisa watano wa serikali pia wamewekewa vikwazo. Tom Andrews mmoja wa maafisa katika ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa, amesema vikwazo hivi vinaonyesha kwamba watu wa Myanmar hawajasahauliwa.