1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya, Marekani waitangazia vikwazo vipya Urusi

23 Februari 2024

Wakati ikitimia miaka miwili tangu Urusi kuivamia Ukraine, Umoja wa Ulaya na Marekani zimetangaza vikwazo vipya dhidi ya Urusi, huku Ukraine yenyewe ikitaka uharakishwaji wa mashitaka ya uhalifu wa kivita.

https://p.dw.com/p/4coPI
Uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine
Moshi ukifuka kwenye majengo ya mji wa Bakhmut baada ya mashambulizi ya vikosi vya Urusi mwezi Aprili 2023.Picha: Libkos/AP/picture alliance

Siku ya Ijumaa (Februari 23), Wizara ya Fedha ya Marekani ilitangaza vikwazo vipya zaidi ya 500 dhidi ya Urusi na sekta yake nzima ya ulinzi, ikiwa hatua kubwa kabisa kuwahi kuchukuliwa kwa wakati mmoja tangu Urusi ilipoivamia Ukraine tarehe 24 Februari 2022.

Hatua hii inakuja wakati tayari pakiwa na hatua nyengine kadhaa zinazojumuisha kukamatwa na kushitakiwa kwa wafanyabiashara wa Kirusi, akiwemo mkuu wa benki ya pili kwa ukubwa nchini Urusi na washirika wao, ambao wamefunguliwa kesi katika majimbo matano tafauti nchini Marekani. 

Soma zaidi: Umoja wa Ulaya kulazimika kuiongezea msaada Ukraine

"Watu wa Marekani na walimwengu wote wanafahamu kwamba hatari ya vita hivi vinavuuka mipaka ya Ukraine. Ikiwa Putin hawajibishwi kwa vifo na uharibifu anaoufanya, ataendelea tu. Na gharama ya hayo kwa Marekani na washirika wetu wa NATO na Ulaya na duniani kote itakuwa kubwa zaidi." Alisema Rais Joe Biden wa Marekani kwenye taarifa yake ya kutangaza vikwazo hivyo.

Vikwazo vya Umoja wa Ulaya

Uamuzi wa Marekani unakwenda sambamba na ule wa Umoja wa Ulaya, ambao nao siku hiyo hiyo ya Ijumaa ulitangaza vikwazo dhidi ya kampuni kadhaa za kigeni kwa tuhuma za kuizuia Urusi bidhaa zinazoweza kutumika kwenye vita dhidi ya Ukraine. 

Josep Borrell
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell.Picha: TOBIAS SCHWARZ/AFP/Getty Images

"Leo tunaongeza makali ya hatua za udhibiti dhidi ya sekta ya ulinzi na jeshi la Urusi. Tunaendelea kuwa wamoja kwenye dhamira yetu ya kuibomoa sekta ya ulinzi ya Urusi na kuisaidia Ukraine kushinda vita vyake halali vya kujilinda." Alisema Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja huo, Joseph Borell.

Soma zaidi: Scholz, Biden waonya juu ya kutoidhinishwa msaada kwa ajili ya vita vya ukraine

Umoja huo wenye mataifa 27 wanachama ulisema kwamba unawawekea pia vikwazo maafisa kadhaa wa serikali ya Urusi, wakiwemo wafanyakazi wa idara ya mahakama na watu wanaodaiwa kuhusika na operesheni ya kuwakamata watoto wa Ukraine na kuwapeleka Urusi ambako wamewekwa kwenye kambi za kijeshi "wanakofundishwa itikadi" inayokinzana na nchi yao.

Ukraine yataka mashitaka ya uhalifu wa kivita kwa Urusi

Ukraine iliiomba jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kuwa waliohusika na uhalifu wa kivita tangu Urusi kuivamia miaka miwili iliyopita, wanawajibishwa. 

Ukraine, Karim Ahmad Khan na Andriy Kostin
Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Karim Ahmad Khan (kulia) akiwa na mwenzake wa Ukraine, Andriy Kosti.Picha: Hennadii Minchenko/Avalon/Photoshot/picture alliance

Akizungumza kwenye kongamano la kimataifa juu ya mashitaka ya uhalifu wa kivita lililokuwa linafanyika katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Ukraine, Andriy Kostin, alisema Urusi imezowea kufanya uhalifu bila kuwajibishwa, kama ambavyo ilifanya Georgia na Syria na sasa inaendelea nchini mwake, Ukraine. 

Ujerumani inashirikiana na Ukraine kwenye kukusanya ushahidi wa uhalifu wa kivita na hadi sasa imesharikodi zaidi ya matukio 500, kwa mujibu wa waziri wake wa sheria, Marco Buschmann.

Vyanzo: dpa, AFP