Umoja wa Ulaya wapendekeza kuimarishwa sera ya uhamiaji
16 Mei 2024Mataifa 15 ya Umoja wa Ulaya yametaka kuimarishwa zaidi kwa sera ya kusimamia suala la kupokea waomba hifadhi na kurahisisha mchakato wa kuwahamisha wahamiaji wasiokuwa na vibali hadi nchi maskini, ikiwa ni pamoja na waliookolea kutoka baharini.
Mapendekezo hayo, yaliyoandikwa kwenye barua iliyokabidhiwa halmashauri ya Umoja wa Ulaya yanajiri chini ya mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wa Bunge la Ulaya, ambapo vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vinavyopinga uhamiaji vinatarajia kupata mafanikio.
Soma: Bunge la EU lapitisha mageuzi makubwa ya sera ya wahamiaji
Barua hiyo inaitaka Halmashauri ya Umoja wa Ulaya ambayo ni taasisi ya maamuzi ya mwisho, kupendekeza njia mpya na suluhu za kuzuia wahamiaji kuingia Ulaya.
Mataifa hayo ni pamoja na Italia na Ugiriki ambayo yanapokea idadi kubwa ya watu wanaofanya safari ya hatari kuvuka Bahari ya Mediterania kuingia Ulaya wengi wakitafuta kuepuka umaskini, vita au mateso, kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.
Aidha mataifa hayo yanahoji kwamba inapaswa kuwa rahisi kuwatuma waomba hifadhi kwa nchi maskini wakati maombi yao ya ulinzi yakitathminiwa.