1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Waasi wa Houthi kutowatumia tena watoto kama wanajeshi

19 Aprili 2022

Umoja wa Mataifa umesema waasi wa Houthi Yemen, wameamua kutowatumia tena watoto kama wanajeshi. Waasi hao wamewatumia maelfu ya watoto kupigana katika vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka saba sasa.

https://p.dw.com/p/4A55K
Jemen Sanaa Kindersoldaten
Picha: Privat

Umoja wa Mataifa umesema waasi hao wametia saini kile kilichoelezewa kama "mpango" wa kufikisha mwisho na kuzuia usajili na kutumiwa kwa watoto katika mapigano, kuuwawa au kujeruhiwa kwao na kushambuliwa kwa shule na hospitali.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema waasi hao wamedhamiria kuwatambua watoto miongoni mwao na kuwaachia huru ndani ya kipindi cha miezi sita ijayo.

Mmoja wa wanadiplomasia wakuu wa Wahouthi Abdul Eluh Hajaar ndiye aliyetia saini makubaliano hayo.

Yemen Huthi Kämpfer
Wapiganaji wa kihouthi nchini YemenPicha: Hani Mohammed/AP Photo/picture-alliance

Serikali ya Yemen nayo yatia saini makubaliano 

Philippe Duamelle ni mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia watoto UNICEF.

"Kwa hiyo tunatazamia kushirikiana na pande zote zinazohusika na mamlaka mjini Sanaa na utekelezaji kamili wa mpango uliotiwa saini. Na tunatazamia kuendelea kufanya kazi na pande zote ili kuboresha usalama kwa watoto nchini Yemen na kumaliza ukiukaji mkubwa wa haki zao," alisema Duamelle.

Umoja wa Mataifa umesema serikali ya Yemen inayotambulika kimataifa na ambayo inafanya kazi uhamishoni, imedhamiria hayo pia katika nyaraka ilizotia saini tangu mwaka 2014.

Umoja wa Mataifa unasema imethibitishwa kwamba watoto 3,500 wamesajiliwa na kupelekwa katika uwanja wa mapambano katika vita yva wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen. Lakini afisa mmoja mwandamizi wa kijeshi wa waasi wa Houthi mwaka 2018 aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba, walikuwa wamewasajili watoto 18,000 katika jeshi lao kufikia mwaka huo. Wanajeshi wa zamani watoto nao walisema hata wavulana walio na umri wa hadi miaka 10 walikuwa wakisajiliwa.

Rais Abed Rabbo Mansour Hadi ajiuzulu

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba zaidi ya watoto 10,200 wameuwawa au kujeruhiwa katika vita hivyo ila haibainiki ni wangapi miongoni walikuwa wanajeshi.

Muungano wa Saudia wakataa kusitisha mapigano Yemen

Pande zinazohasimiana nchini Yemen mapema mwezi huu zilikubaliana kusitisha mapigano kote nchini humo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka sita. Makubaliano hayo ya kuweka chini silaha yalikuwa yananuiwa kuanza katika mwezi wa Ramadhani na uliibua matumaini ya kupatikana kwa amani.

Rais wa Yemen Abed Rabbo Mansour Hadi alijiuzulu wiki iliyopita na kusema baraza jipya la rais litaiendesha serikali hiyo na kuongoza mazungumzo na Wahouthi.

Chanzo: APE