UN yaelezea wasiwasi kuhusu hali katika eneo la Tigray
3 Februari 2021Taarifa ya Jumanne ya Guterres imeelezea kuwa ana wasiwasi mkubwa kuhusu hali ilivyo katika eneo la Tigray nchini Ethiopia, akisisitiza haja ya ushirikiano kati ya serikali ya Ethiopia na Umoja wa Mataifa ili kupunguza mateso kwa raia.
Katibu huyo mkuu pia alipongeza mapokezi mazuri ya serikali ya Ethiopia wakati wa ziara za hivi karibuni ya Kamishna Mkuu wa Shirika linalowashughulikia Wakimbizi la Umoja huo UNHCR, Filippo Grandi, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Ulinzi na Usalama,GillesMichaud, na mkurugenzi mtendaji wa Mpango wa Chakula Duniani WFP, David Beasley.
Kulingana na wanadiplomasia, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana leo kujadili suala hilo. Wanadiplomasia hao wanasema kuwa Ireland, Estonia, Ufaransa, Norway, Uingereza na Marekani zilitaka kuandaliwa kwa mkutano huo wa faragha.
Kambi mbili za wakimbizi kaskazini mwa Tigray, Hitsats na Shimelba, ambazo ziko karibu na mzozo huo, bado haziwezi kufikiwa na shirika hilo la UNHCR au shirika la Ethiopia linalosimamia misaada kwa wakimbizi hao, ARRA. Umoja wa Mataifa una wasiwasi hasa kuhusu uwezekano wa mauaji au utekaji nyara unaofanywa na wanajeshi wa Eritrea, ambao uwepo wao huko Tigray unaripotiwa sana, licha ya kukanushwa na serikali ya Ethiopia.
Huku hayo yakijiri, katika taarifa ya pamoja siku ya Jumanne, vyama vitatu vya upinzani Tigray: Indepence Party - TIP, Salsay Weyane Tigray na Great Tigray Baytona, vimesema kuwa raia elfu 52 wanaowajumuisha watoto, wanawake, vijana, wazee na makasisi wamechinjwa ovyo ovyo. Hata hivyo, taarifa hiyo haikusema yalipotokea makadirio hayo na vyama hivyo havikuweza kufikiwa kwa haraka. Mawasiliano kwenye eneo hilo yanapatikana kwa tabu na ni vigumu kuthibitisha madai hayo.
Vyama hivyo vya upinzani vinasema kuwa jamii ya kimataifa inapaswa kuhakikisha kuondolewa mara moja kwa wapiganaji ikiwa ni pamoja na wanajeshi kutoka nchi jirani ya Eritrea, ambao wanaoshuhudia wanasema wanaunga mkono wanajeshi wa serikali ya Ethiopia.