1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

UN yaitaka Iran kusitisha kamatakamata ya waandamanaji

24 Novemba 2022

Wanadiplomasia wa mataifa ya Magharibi na mkuu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa serikali ya Iran kusitisha kamatakamata ya waandamanaji iliyosababisha umwagikaji wa damu nchini humo.

https://p.dw.com/p/4K0x6
Volker Turk, (kwenye picha) ni mkuu wa tume ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa.
Volker Turk, (kwenye picha) ni mkuu wa tume ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa.Picha: Martial Trezzini/KEYSTONE/picture alliance

Wameyasema hayo katika kikao maalum cha Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva, Uswisi, kilichokuwa kinajadili ombi la kuchunguzwa zaidi kwa hali ya haki za binadamu inayozidi kuwa mbaya nchini humo.

Kikao hicho cha Geneva ndio juhudi za hivi majuzi za kimataifa kuiwekea shinikizo Iran ambayo hatua yake ya kuwakamata waandamanaji imeipelekea nchi hiyo tayari kuwekewa vikwazo vya kimataifa na hatua zengine kuchukuliwa dhidi yake.

Iran yazishutumu nchi za kigeni kwa machafuko yanayoendelea

Mkuu wa Umoja wa mataifa wa haki za binadamu Volker Turk anasema Iran kwa sasa inakabiliwa na mzozo kamili wa haki za binadamu huku watu 14,000 wakiwa wamekamatwa wakiwemo watoto.

Baraza hilo la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 47, linatarajiwa kujadili pendekezo la kuunda kikosi cha wachunguzi huru watakaoitazama kwa karibu hali ya haki nchini Iran. Pendekezo hilo liliwasilishwa na Ujerumani na Iceland na limeungwa mkono na nchi nyengine nyingi.

"Mheshimiwa rais na wanadiplomasia wenzangu, ndio maana kwa sasa tunapendekeza kubuniwa kwa kikosi huru na kisichoegemea upande wowote kuchunguza ukiukaji huu wa haki za binadamu ili wahusika wachukuliwa hatua, kwasababu kutokujali kunazuia haki, haki kwa dada zetu, haki kwa watoto wetu na haki kwa kina mama zetu," amesema Baerbock.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, karibu watu 300 wameuwawa katika maandamano nchini Iran tangu Septemba.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, karibu watu 300 wameuwawa katika maandamano nchini Iran tangu Septemba.Picha: Idil Toffolo/Pacific Press/picture alliance

Pendekezo hilo la kubuniwa kwa kikosi hicho litapigiwa kura baadae leo katika baraza hilo la haki la Umoja wa Mataifa.

1,000 washitakiwa kwa kuandamana Iran

Katika jawabu la moja kwa moja, mjumbe wa Iran Khadijeh Karimi amepinga na kusimama na msimamo wa nchi yake akisema mpango huo wa Magharibi umechochea kisiasa.

"Kwa bahati mbaya baada ya kifo cha Mahsa Amini, hatua zinazohitajika zilichukuliwa ikiwemo kubuniwa kwa tume huru ya uchunguzi ya bunge na pia kikosi cha uchunguzi wa kitabibu. Ila kabla tangazo rasmi la matokeo ya uchunguzi, mamlaka kadhaa za nchi za Magharibi zinazoegemea upande mmoja pamoja na hatua yao ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran, zilipelekea mikusanyiko ya amani kugeuka na kuwa machafuko na huo ukawa msingi wa mashambulizi ya kigaidi katika miji kadhaa," amesema Karimi.

Umoja wa Mataifa wiki hii ulisema karibu watu 300 wameuwawa katika maandamano hayo tangu Septemba na wengine 40 kupoteza maisha katika maeneo yanayokaliwa na idadi kubwa ya Wakurdi tangu wiki iliyopita.

Vyanzo: Reuters/AP