1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yatafakari vikwazo Sudan Kusini

Kabogo Grace Patricla24 Aprili 2014

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linafikiria kuweka vikwazo dhidi ya makundi yanayopigana nchini Sudan Kusini, huku rais wa nchi hiyo Salva Kiir, akimfukuza kazi mkuu wa majeshi, baada ya waasi kuutwa mji wa Bentiu.

https://p.dw.com/p/1Bnj5
Safari kunako mashakani: Raia wa Sudan Kusini wakikimbia machafuko katika mji wa Bentiu.
Safari kunako mashakani: Raia wa Sudan Kusini wakikimbia machafuko katika mji wa Bentiu.Picha: Reuters

Mkuu wa shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa, Herve Ladsous na msaidizi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binaadamu, Ivan Simonovic, wamewapa maelezo mafupi wajumbe 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya kusambaa kwa mashambulizi ya raia, yakiwemo mauaji ya kikabila kwenye mji wa Bentui wenye utajiri wa mafuta pamoja na mauaji ya watu kadhaa walioomba hifadhi kwenye kambi ya kikosi cha kulinda amani cha umoja huo kilichoko mjini Bor.

Askari wa Umoja wa Mataifa akilinda doria Karibu na eneo yalikofanyika mauaji ya karibu watu 200 katika mji wa Bentiu.
Askari wa Umoja wa Mataifa akilinda doria Karibu na eneo yalikofanyika mauaji ya karibu watu 200 katika mji wa Bentiu.Picha: Reuters

Ladsous amesema mauaji ya raia wasio na hatia yataendelea iwapo pande zinazopigana hazitoweka chini silaha na kujikita zaidi katika mazungumzo yenye kuleta tija. Amesema Umoja wa Mataifa unafanya kila uwezalo, kuwalinda raia wanaokimbia vita, lakini ikumbukwe kuwa jukumu la kwanza la kuwalinda raia liko mikononi mwa serikali. Ladsous ameonya kuwa vita hivyo vinaweza kuwa janga la kibinaadamu, iwapo havizasitishwa.

Wanachama waunga mkono vikwazo

Balozi wa Nigeria kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Joy Ogwu, ambaye ndiyee rais wa baraza hilo kwa mwezi huu wa Aprili, amesema wanachama wanaunga mkono vikwazo kuwekwa dhidi ya Sudan Kusini.

Tayari Marekani na Umoja wa Ulaya zimetishia kuiwekea vikwazo Sudan Kusini. Mwanzoni mwa mwezi huu, Rais Barack Obama aliidhinisha vikwazo kadhaa dhidi ya wale wote wanaohusika na kukiuka haki za binaadamu Sudan Kusini au kudhoofisha demokrasia na kuzuia mchakato wa amani.

Mkuu wa majeshi atimuliwa

Wakati hayo yakijiri, Rais Salva Kiir amemfukuza kazi mkuu wa majeshi wa Sudan Kusini, Jenerali James Hoth Mai na nafasi yake kuzibwa na Jenerali Paul Malong. Hata hivyo, sababu za kufukuzwa hazijatangazwa, ingawa duru za karibu zinaeleza kuwa huenda sababu ikawa kushindwa kwa jeshi kuudhibiti mji wa Bentiu ulioko kaskazini mwa nchi hiyo.

Askari wa Umoja wa Mataifa akilinda doria Karibu na eneo yalikofanyika mauaji y akaribu watu 200 katika mji wa Bentiu.
Askari wa Sudan wakikagua mabegi ya raia wa Sudan Kusini wanaotafuta hifadhi nchini Sudan.Picha: Reuters

Rais Kiir pia amemfukuza kazi mkuu wa ujasusi, Jenerali Paul Mach na nafasi yake kuchukuliwa na Jenerali Marial Nour Jok. Jeshi la Sudan Kusini limekuwa likipigana na waasi tangu Disemba 15 mwaka uliopita, lakini mzozo huo umegeuka na kuwa wa kikabila kati ya kabila la Kiir la Dinka na kabila la Nuer, la kiongozi wa waasi, Riek Machar.

Wakati huo huo, kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusiniu, kimeishutumu serikali ya nchi hiyo kwa kueneza taarifa za uongo kwamba kambi ya umoja huo karibu na eneo yalipotokea mauaji, ilikataa kuwahifadhi wahanga.

Shirika la kimataifa la haki za binaadamu la Human Rights Watch, limelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchunguza mauaji ya Bentiu na vifo vingine vilivyotokea mwanzoni mwa mwezi huu kwenye mji wa Bor.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE,APE
Mhariri: Iddi Ssessanga