UNRWA kusitisha huduma zake Gaza kutokana na uhaba wa mafuta
14 Novemba 2023Mkuu wa shirika hilo Thomas White aliandika kupitia ukurasa wa X kwamba UNRWA, imekuwa ikitumia mafuta kutoka katika hifadhi yake, lakini nako mafuta yamewaishia. Afisa huyo amesema hakuna mafuta yaliyoruhusiwa kuingia Gaza tangu Oktoba 7, wakati Hamas walipofanya mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Israel.
Wizara ya Afya inayoendeshwa na Hamas pia ilisema mapema siku ya Jumatatu kwamba hospitali zote kaskazini mwa Gaza hazifanyi kazi tena kutokana na uhaba wa mafuta.
Soma pia: UN yawakumbuka watumishi wake waliouawa kwenye vita vya Mashariki ya Kati
Katika hatua nyingine, Rais wa Marekani Joe Biden ametoa wito kwa Israel wa kuilinda hospitali kubwa ya Al-Shifa katika Ukanda wa Gaza. Biden ametoa wito huo wakati shirika la afya ulimwenguni WHO likisema hospitali hiyo haifanyi kazi tena.
Wafanyakazi katika hospitali hiyo wamedai kuzingirwa, baada ya kituo hicho kushambuliwa mara kadhaa kwa mabomu. Wamesema Israel inawapiga risasi watu wanaotoka nje ya jengo hilo. Madai hayo yamekanushwa na Israel inayodai kwamba wanamgambo wa Hamas wanatumia mtandao wa mahandaki ulio chini ya hospitali.