Urusi, Ukraine zabadilishana mamia ya wafungwa
4 Januari 2024Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema imekabidhiwa wanajeshi wake 248 na Ukraine, huku upande wa Ukraine ukisema umewarejesha nyumbani watu 230, kati yao wakiwemo raia sita, yakiwe mabadiliko makubwa kabisa ya wafungwa wa kivita kuwahi kufanyika baina yao.
Kyrylo Budanov, mkuu wa Intelejensia katika jeshi la Ukraine, alisema jukumu la Umoja wa Falme za Kiarabu lilikuwa kubwa sana kwenye kufanikisha mabadilishano hayo ya Jumatano (Januari 3).
"Baada ya muda mrefu sana, tumefanikiwa japo kwa shida sana kutimiza makubaliano haya." Alisema mkuu huyo.
Soma zaidi: Ukraine na Urusi zabadilishana wafungwa kwa mara nyingine tangu vita vilipozuka Februari 2022
Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Umoja wa Falme za Kiarabu ulisema kwenye taarifa yake kwamba "kufanikiwa kwa juhudi hizo kulitokana na urafiki uliopo" kati yake na pande zote mbili, Moscow na Kiev.
Taifa hilo la Kiarabu liliziomba pande hizo zikubali kumaliza vita hivyo kwa njia za amani na pia kuahidi kuendeleza misaada ya kibinaadamu kwao.
Wafungwa wawasili makwao
Video iliyotolewa na mamlaka za Ukraine inawaonesha wafungwa wanaorejea nyumbani wakipeperusha bendera za nchi yao wakiwa kwenye mabasi na huku wakiimba wimbo wa taifa na mayowe na kuitukuza Ukraine.
Wengi wao, ingawa si wote, walionekana wakiwa na hali nzuri kiafya. Mmoja wao alipaza sauti akisema: "Tumerudi kwetu. Hamukutusahau!"
Soma zaidi: NATO kuzisaidia nchi wanachama kununua makombora ya Patriot
Wizara ya Ulinzi ya Urusi nayo ilitowa video kama hiyo ya wafungwa wenye sare wakiwasili kwa mabasi kwenye mji wa mpakani wa Belgorod. Mmoja wao alisema: "Nitafika nyumbani kwangu takribani masaa matano kutoka sasa, na kutakuwa na sherehe kubwa."
Volodmyr aapa kutanuwa "mfuko wa mabadilishano"
Rais Volodymyr Zelenskiy ameiita jana kuwa siku kubwa kwa Ukraine, huku akiapa kuendelea kufanya kila jitihada ya mabadilishano zaidi ya wafungwa kwa kutanuwa kile alichokiita "mfuko wa mabadilishano" - kwa kuwateka nyara wanajeshi wengi zaidi wa Urusi ili kuwabadilisha na wale waliotekwa na Moscow.
Baadhi ya wanajeshij wa Ukraine walioachiliwa siku ya Jumatano walikuwa wameshikiliwa tangu mwaka 2022. Miongoni mwao walikuwa wale waliopigana vita vikali kutetea Kisiwa cha Nyoka cha Ukraine na pia mji wa Mariupol.
Soma zaidi: Urusi: Ukraine yashambulia tena Belgorod kwa makombora-droni
Licha ya kutokuwapo mazungumzo ya kuvikomesha vita hivyo vinavyoingia mwaka wake wa pili sasa, Kyiv na Moscow zimeshafanya mabadilishano 49 ya wafungwa tangu kwenye miezi ya awali ya uvamizi wa Urusi mwezi Februari 2022.
Mabadilishano ya mwisho kabla ya jana yalikuwa ya mwezi Agosti 2023.