Urusi yaendeleza mashambulizi ya makombora Ukraine
22 Agosti 2022Katika taarifa yake ya kila siku Mkuu wa majeshi ya Ukraine amesema vikosi vya Urusi vimesababisha uharibifu kutokana na mashambulizi ya makombora katika jimbo la Bakhmut lililoko mashariki mwa Ukraine, huku roketi kadhaa zikirushwa kwenye maeneo ya makaazi ya Soledar, Zaytseve na Bilogorivka.
Mashambulizi mengine ya makombora yamefanyika kwenye eneo la Nikopol, mji ulio karibu na Zaporizhizhia, ambako kuna kinu kikubwa kabisa cha nishati ya nyuklia barani Ulaya.
Mashambulizi yasababisha kukatika umeme Nikopol
Gavana wa jimbo la Dnipropetrovsk amesema Nikopol imeshambuliwa kwa makombora katika matukio matano tofauti. Amesema roketi 25 zimeushambulia mji huo na kusababisha moto mkubwa katika eneo la viwanda na kuchangia kukatika kwa umeme unaotumiwa na wakaazi 300,000.
Aidha, mwishoni mwa juma lililopita makombora pia yalishambulia karibu na bandari ya Odesa iliyoko katika Bahari Nyeusi. Urusi kwa upande wake imesema makombora aina ya Kalibr yameharibu ghala la silaha lililokuwa na mifumo ya kisasa ya makombora yaliyotengenezwa na Marekani aina ya HIMARS kusini mashariki mwa jimbo la Odesa.
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ameitaka nchi yake kujiweka tayari akisema Urusi huenda ikajaribu kufanya mashambulizi mabaya kabla ya Jumatano, ambayo ni siku ya uhuru wa Ukraine kutoka kwa utawala wa Kisovieti na pia ni nusu mwaka tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 24. ''Kwa siku 180, takribani miezi sita, idadi kubwa ya watu wetu haina shaka kwamba tutapata ushindi wa Ukraine. Tumeungana, tunajiamini zaidi sasa kuliko tulivyokuwa katika miongo mingi iliyopita,'' alifafanua Zelensky.
Ukraine imezungumzia vitisho na viongozi kadhaa
Zelensky amesema iwapo Urusi itaendelea na mipango yake ya kujaribu kuwateka watetezi wa Ukraine kwenye mji wa Mariupol, basi itakuwa imekiuka sheria za kimataifa na kujiondoa yenyewe kwenye mazungumzo. Kiongozi huyo amesema amejadiliana kuhusu ''vitisho vyote'' na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron pamoja na viongozi wengine akiwemo Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.
Huku hayo yakijiri, ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson imesema kuwa viongozi wa Uingereza, Marekani, Ufaransa na Ujerumani wametoa wito wa pamoja wa kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama unakuwepo kwenye maeneo yenye vinu vya nyuklia nchini Ukraine.
Wakati huo huo, binti wa mshirika wa karibu wa Rais wa Urusi Vladmir Putin, ambaye ana misimamo mikali na anatetea uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, Alexander Dugin ameuawa katika shambulizi la bomu lililotegwa ndani ya gari. Kamati ya upelelezi ya Urusi imesema kuwa binti huyo, Daria Dugina, alikufa akiwa ndani ya gari aina ya Toyota Land Cruiser baada ya gari hilo kuripuka karibu na kijiji cha Bolshie Vyzyomy nje kidogo ya mji wa Moscow.
(DPA, AFP, Reuters)