1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi yaivurumishia mvua ya makombora Ukraine

29 Desemba 2023

Watu wasiopungua 10 wameuawa na makumi kadhaa kujeruhiwa katika wimbi la mashambulizi ya Urusi dhidi ya miji mbalimbali nchini Ukraine mapema leo, huku maafisa wakitarajia idadi hiyo kuongezeka.

https://p.dw.com/p/4aguX
Kyiv, Ukraine | Jengo likiteketea kwa moto baada ya kupigwa na kombora la Urusi.
Moja ya jengo katika mji wa Kyiv likiwaka moto baada ya kupigwa na kombora la Urusi, yaliovurumishwa usiku kucha.Picha: Ukrainian Emergency Service/AP/picture alliance

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, amesema Urusi imerusha takribani makombora 110 leo Ijumaa, katika mmoja ya mashambulizi yake makubwa zaidi ya angani dhidi ya Ukraine, huku akiongeza kuwa mengi ya makombora hayo yamedunguliwa na mifumo ya ulinzi wa anga.

Msemaji wa jeshi la anga la Ukraine Yurii Ihnat amesema mashambulizi ya leo yamehusisha aina zote za makombora, ikiwemo makombora ya kisasa ya Kinzhal, makombora ya masafa marefu chapa S-300, pamoja na droni za masafa marefu zilizotengenezwa nchini Iran.

Ameongeza kuwa ndege 18 za mashambulizi ya kimkakati pia zilitumwa kushiriki mashambulizi hayo. Ving'ora vya tahadhari vimelia kote nchini humo, huku uharibifu ukiripotiwa katika miji ya Kharkiv, Lviv, Dnipro na Kiev.

Soma pia:Zelensky atoa wito wa ushirikiano dhidi ya vita vya Urusi nchini Ukraine

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, kulikuwepo na milipuko Odessa, Khmelnytskyi na Zaporizhzhya, ambapo maafisa wamezungumzia vifo visivyopungua 10 na zaidi ya dazeni tatu waliojeruhiwa kote nchini humo.

Kisasi cha meli yake ya kivita?

Mashambulizi hayo yaliodumu kwa takribani saa 18 yalioanza Alhamisi na kuendelea usiku kucha, yamekuja siku chache baada ya Ukraine kuishambulia meli ya kivita ya Urusi katika bandari ya Feodosia katika rasi ya Crimea, katika pigo kubwa kwa jeshi la majini la Urusi.

Baadhi ya Waukraine waamua kutoroka kuliko kupigana na Urusi

Ukraine ilisema jeshi lake la angaliliiharibu meli ya kutua ndege ya Novocherkassk, huku Rais Zelenskiy akitania kwenye mtandao wa kijamii kwamba meli hiyo sasa imejiunga na "kundi la manowari za Urusi zilizoko chini ya Bahari Nyeusi."

Ikulu ya Kremlin imesema waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu alimuarifu rais Vladmir Putin kuhusu uharibifu uliosababishwa kwa meli yao. Wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema meli hiyo iliharibiwa na makombora ya kuongozwa.

Soma pia:Urusi: Mataifa ya Magharibi yapendekeza Moscow kufanya majadiliano ya amani na Ukraine

Kwa mujibu wa jeshi la anga la Ukraine, mashambulizi makubwa zaidi yaliopita yalikuwa mwezi Novemba 2022, wakati ambapo Urusi ilirusha makombora 96 dhidi ya Ukraine.

Mashambulizi ya leo yamekujwa wakati mapigano kwenye safu ya mbele yamekwama kwa sehemu kubwa kutokana na hali ya hewa ya baridi kali, na baada ya kushindwa kwa operesheni ya msimu wa joto ya Ukraine kurejesha maeneo yaliotwaliwa na Urusi.