1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usitishaji wa mapigano Gaza waonekana kuheshimiwa

14 Machi 2014

Israel inasema usimamishaji mapigano uliotangazwa na wapiganaji wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza kati yao na Israel umeanza kutekelezwa, licha ya makundi mengine kurusha makombora.

https://p.dw.com/p/1BPbu
Moshi na moto ukionekana kutokea Gaza baada ya mashambulizi ya anga ya Israel mwishoni mwa mwaka 2012.
Moshi na moto ukionekana kutokea Gaza baada ya mashambulizi ya anga ya Israel mwishoni mwa mwaka 2012.Picha: Jack Guez/AFP/Getty Images

Jeshi la Israel limeripoti kwamba kufikia asubuhi ya Ijumaa (tarehe 14 Machi 2014) hakukuwa na mashambulizi mapya kutokea Gaza na hivyo kuashiria kuwa mkasa wa piga-nikupige kati yake na wanamgambo wa Kipalestina umesimama.

Kufikia majira ya saa 2:00 asubuhi, msemaji wa jeshi hilo alithibitisha kwamba usiku mzima ulipita salama. Mapigano hayo yaliyodumu kwa siku mbili yalikuwa mabaya kabisa kati ya pande hizo mbili tangu mwishoni mwa mwaka 2012.

Mkuu wa kundi la wanamgambo la Islamic Jihad, Khalid al-Batch, alikuwa amesema jioni ya jana kwamba majibizano ya maroketi kati yao na Israel yamemalizika kwa makubaliano yaliyosimamiwa na Misri. Al-Batch alisema kadiri ambavyo Israel itaheshimu makubaliano hayo, nao pia watayaheshimu.

Abbas azilaani pande zote mbili

Mapema siku ya Alhamis, wakati akikutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, Rais Mahmoud Abbas wa Palestina alizilaumu pande zote mbili kwenye mzozo huo, na kuionya Israel kwamba kuendelea kwake na mashambulizi dhidi ya Wapalestina kunahatarisha mazungumzo ya amani kati yao, ambayo tangu hapo yameshakwama.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron (kushoto) na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron (kushoto) na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina.Picha: dapd

"Jeshi la uvamizi la Israel muda mchache uliopita limewauwa kinyama Wapalestina watatu kwenye Ukingo wa Magharibi na watatu zaidi huko Gaza. Hatusikii serikali ya Israel ikilaani vitendo kama hivyo. Jana kulikuwa na maroketi kutoka Gaza na Israel ikalipiza kisasi. Tunalaani mashambulizi na kuendelea kwa hatua za kijeshi katika hali yoyote iwayo, yakiwemo maroketi." Alisema Rais Abbas katika mkutano wake na waandishi wa habari akiwa na Waziri Mkuu Cameron.

Usitishaji huo wa mapigano ulitazamiwa kuanza kutekelezwa saa nane ya mchana, kwa saa za Mashariki ya Kati, lakini hadi jioni ya jana kuliripotiwa makombora kuendelea kuvurumishwa, na hadi hapo maafisa wa Israel walikataa kuthibitisha ikiwa nchi hiyo imekubaliana na pendekezo lililotolewa na Misri.

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Israel aliliambia shirika la habari la AFP kwamba alikuwa hayafahamu makubaliano hayo, na kwamba mashambulizi yoyote kutoka Gaza yangelijibiwa kwa hatua kali zaidi kutoka Israel.

Israel kuendelea 'kujibu mashambulizi'

Muda mchache baada ya kutangaza kuwa makombora manne yamerushwa kutokea Gaza, hata baada ya muda wa kutekelezwa kwa makubaliano hayo kuanza, jeshi la Israel lilisema kuwa lilijibu mashambulizi kwa kulenga maeneo manne kusini na mengine matatu kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

Wapalestina wakiziswalia maiti za wapiganaji watatu wa Islamic Jihad waliouwa na mashambulizi ya anga ya Israel tarehe 11 Machi 2014.
Wapalestina wakiziswalia maiti za wapiganaji watatu wa Islamic Jihad waliouwa na mashambulizi ya anga ya Israel tarehe 11 Machi 2014.Picha: Reuters

Hamas imeilaumu Israel kuwa ndio chanzo cha mapigano haya mapya, baada ya jeshi la nchi hiyo kuwauwa wapiganaji watatu wa kundi la Islamic Jihad hapo juzi.

Kwa ujumla, katika mapigano hayo ya siku mbili, Israel ilifanya mashambulizi 29 kutokea angani na kurusha maroketi kadhaa kuelekea Gaza, huku kundi la Islamic Jihad likirusha maroketi 60.

Hakuna upande ulioripoti vifo hadi sasa, ingawa bado miji ya Ashkelon na Ashdod iliyo kusini mwa Israel iko kwenye hali ya tahadhari, licha ya tangazo hilo la kukomeshwa kwa mapigano.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba