Jeshi kumshitaki Bazoum kwa uhaini
14 Agosti 2023Utawala huo wa kijeshi umesema tayari umekusanya ushahidi utakaotumika kumshitaki Bazoum pamoja na washirika wake wa ndani na wa nje kwenye vyombo vinavyoaminika vya kitaifa na kimataifa, hii ikiwa ni kulingana na taarifa iliyosomwa na Kanali Meja Amadou Abdramane kupitia televisheni ya taifa.
Bazoumu bado anazuiliwa kwenye kasri la rais, pamoja na mtoto wake wa kiume na mkewe, tangu kulipofanyika mapinduzi hayo yapata wiki ya tatu sasa.
Taarifa hiyo ya kijeshi imesema Bazoum bado anaweza kuwasiliana na watu wa nje kwa kuwa hawajazuia mawasiliano kwenye kasri hilo la rais na bado anakutana na daktari wake kila wakati na kuongeza kuwa hata Jumamosi hii alikutana nae na taarifa ya daktari huyo ilisema familia yote haikuwa na tatizo lolote la kiafya.
Soma Zaidi: Rais aliyepinduliwa Niger atembelewa na daktari
Kiongozi huyo aliyeondolewa amesema alikuwa anashikiliwa mateka bila ya umeme na amekuwa akilishwa wali na tambi tu.
Viongozi wa kijeshi walaani vikwazo vya ECOWAS.
Katika hatua nyingine, viongozi hao wa mapinduzi wamekosoa vikali vikwazo walivyoviita visivyo vya kiutu, vya kinyama na vinavyofedhehesha walivyowekewa na Jumuiya ya Maendeleo Afrika Magharibi, ECOWAS.
Mmoja ya viongozi hao Kanali Meja Amadou Abdramane amesema kupitia taarifa iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa, watu wa Niger wameathiriwa vibaya na vikwazo hivyo vya ECOWAS na kuongeza kuwa raia wanakosa dawa, chakula na hata huduma ya umeme, kama ambavyo fundi nguo huyu ambaye hakutaja jina lake anavyolalama:
"Tulizoea kufanya kazi kuanzia saa mbili asubuhi hadi usiku wa manane, lakini sasa haiwezekani. Kwa siku tunapata umeme angalau kwa saa moja na nusu na ni vigumu sana kuzalisha katika mazingira kama haya."
ECOWAS imezuia miamala ya kifedha na usambazaji wa umeme na kufunga mipaka na Niger, taifa lisilo na bandari, pamoja na kuzuia uagizaji wa bidhaa licha ya mahitaji yake makubwa.
Utawala wa kijeshi waonyesha nia ya suluhu ya kidiplomasia.
Hapo kabla, kiongozi wa utawala wa kijeshi nchini humo alisema yuko tayari kwa suluhu ya kidiplomasia kwenye mzozo baina yake na Jumuiya hiyo ya ECOWAS.
Mkuu wa ujumbe wa kidini Sheikh Bala Lau, alisema jana Jumapili kwamba kiongozi huyo Jenerali Abdourahamane Tiani alisema milango ipo wazi ya kuusuluhisha mvutano kwa njia ya kidiplomasia na amani.
Tiani alitoa matamshi hayo hayo siku moja baada ya ujumbe wa Kiislamu kutoka Nigeria kufanya nao mazungumzo, katika mji mkuu Niamey.
Kulingana na Sheikh Lau, Tiani alisema mapinduzi hayo yalikuwa na nia njema na wahusika walipanga kuepusha kitisho ambacho kingeweza kuiathiri si tu Niger, bali pia Nigeria na kulalamika kwamba ECOWAS iliamua tu kuchukua hatua ya kuwawekea ukomo wa kumuachia Bazoum, bila hata ya kuwasikiliza.
Soma Zaidi: Maelfu ya watu waandamana Niger kupinga vikwazo vya ECOWAS
Kiongozi huyo aidha aliomba radhi kwa kutousikiliza vya kutosha ujumbe wa ECOWAS uliotumwa Niger, chini ya kiongozi wa zamani wa Nigeria Abdulsalami Abubakar, akisema hatua hiyo ilitokana na hasira juu ya uamuzi huo.
Julai 30, ECOWAS iliupa siku saba uongozi huo kumrejesha Bazoum au kukabiliwa na uwezekano wa matumizi ya nguvu, lakini muda huo uliisha bila watawala hao kumuachia.