Uturuki yaitaka Denmark kuchukua hatua uchomaji Quran
29 Julai 2023Waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki Hakan Fidan ameitolea wito Denmark kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya uchomaji moto wa kitabu kitakatifu kwa Waislamu cha Quran.
Katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na waziri wa mambo ya nje wa Denmark Lars Lokke Rasmussen, Fidan amesema kuwa, haikubaliki kuruhusu vitendo vya aina hiyo kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza. Hivi karibuni, mwanamume mmoja alichoma kurasa za Quranmbele ya Msikiti wa Stockholm wakati wa maandamano yaliyoidhinishwa na mamlaka ya Sweden.
Kitendo hicho kimelaaniwa na nchi nyingi za Kiislamu na kukishutumu kuwa ni kitendo cha chuki na uchochezi. Naye kiongozi wa kundi la wapiganaji la Hezbollah Hassan Nasrallah amesema ikiwa serikali za mataifa ya Kiislamu hazitachukua hatua dhidi ya nchi zinazoruhusu kuchafuliwa kwa Quran, basi Waislamu wanapaswa kuwaadhibu wale wanaowezesha mashambulizi hayo..