Uzuiaji wa nafaka za Ukraine wahatarisha maisha ya mamilioni
8 Juni 2022Kusini mwa Ukraine, ni uwanja mwingine wa mapambano makali. Maafisa wa Ukraine wamesema vikosi vya Urusi vimeshambulia vituo vya kilimo ikiwemo mabohari. Hali inayozusha wasiwasi zaidi kuhusu hali ya njaa inayoanza kujitokeza katika mataifa maskini.
Mapema leo, waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu alikuwa mwenyeji wa mkutano kati yake na mwenzake kutoka Urusi Sergei Lavrovkatika mazungumzo yaliyolenga mpango wa Umoja wa Mataifa wa kufungua njia katika bahari Nyeusi, kuwezesha usafirishaji na uuzaji wa nafaka za Ukraine, ambazo zimezuia katika bandari kufuatia mzingiro wa Urusi. Sergei alipinga taarifa kwamba hatua ya Urusi kuzuia nafaka za Ukraine kutosafirishwa imechangia uhaba wa chakula ulimwenguni.
"Hali ya sasa ya nafaka za Ukrain haina uhusiano wowote na mgogoro wa uhaba wa chakula ulimwenguni. Rais Vladimir Putin alizungumzia hilo kwa upana kwenye mahojiano wiki moja iliyopita. Hali kamili iliangaziwa na kila aliyetaka kusikiliza alisikia," amesema Lavrov.
Merkel atetea urathi wake wa Urusi, asema hataomba radhi
Kwingineko rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema umoja wake unapaswa kuuvunja uwongo wa Urusi wa kuelekeza lawama kwa nchi za magharibi kuchangia tatizo la uhaba wa chakula ulimwenguni.
Akilihutubia bunge la Ulaya mjini Strasbourg Ufaransa leo, Von der Leyen amesema Urusi sasa inatumia suala la uhaba wa chakula ulimwenguni kama sehemu ya ala zake za kivita, jambo ambalo hawawezi kukubali.
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kwamba vita vitafanya hali ya njaa ulimwenguni kuwa mbaya zaidi hasa ikizingatiwa nchi 54 za Afrika huagiza karibu nusu ya ngano zao kutoka Ukraine na Urusi.
Ukraine: Zelenskiy atembelea vikosi vya msitari wa mbele
Waziri wa mambo ya nje wa Italia Luigi Di Maio aliyekuwa mwenyeji wa mkutano wa mawaziri wenzake wa kanda ya Mediterania amesema huenda mamilioni ya watu wakafa kwa njaa ikiwa Urusi haitaacha huru bandari za Ukraine.
Ukraine ilikuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza ulimwenguni kote katika kilimo na biashara ya ngano.
Sergei alisema ni sharti Ukraine iondoe mabomu kwenye bandari zake, takwa ambalo Ukraine inahofia litaiacha katika hatari ya mashambulizi kutoka baharini.
Urusi na Ukraine zinashutumiana kutega mabomu majini katika pwani za bahari Nyeusi, jambo linalozusha wasiwasi wa kiusalama hata mazungumzo hayo ya kufungua njia kusafirisha nafaka yakiendelea.
Vita vya Urusi na Ukraine vyaingia siku 100
Kulingana na ripoti ya shirika la habari la Ujerumani DPA, mkutano kati ya Cavusoglu na Lavrov haukupata suluhisho kwa sababu hakukuwa na mwakilishi wa Ukraine kwenye mazungumzo hayo.
Katika tukio jingine, shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Urusi TASS limeripoti kwamba zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Ukraine waliokamatwa na vikosi vya Urusi mjini Mariupol wamepelekwa Urusi kama wafungwa wa kivita kufunguliwa mashtaka.
(DPAE;RTRE, AFPE)