Vikosi tiifu kwa Roble vyakusanyika karibu na Ikulu Somalia
29 Desemba 2021Mpiga picha wa shirika la habari la Reuters amesema mbali na kukusanyika vikosi vya usalama havikuchukua hatua yoyote kufikia Jumanne jioni. Lakini mkusanyiko huo ulizua hofu ya kutokea mzozo kati ya vikosi tiifu kwa viongozi wawili hao.
Canab Osman, mama wa watoto saba na anaendesha shughuli za duka la vyakula na bidhaa ndogondogo na mboga mboga ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa wanajeshi wameweka kambi katika kijiji chao, karibu na Villa Somalia, ambayo ni ikulu ya rais nje kidogo ya mji mkuu, Mogadishu.
Mkazi mwingine na mzee wa eneo hilo, Farah Ali, ameambia Reuters kuwa vikosi vya usalama vilivyokusanyika katika eneo hilo vilikuwa na malori yenye silaha za mizinga.
Soma pia:Washirika wa Somalia waelezea wasiwasi wa mzozo wa kisiasa
Njia ndefu kuelekea uchaguzi
Mohamed Roble ameiita hatua ya Rais Mohamed ya kumsimamisha kazi kuwa ni jaribio la mapinduzi. Taarifa iliotolewa na Marekani, ambayo imekuwa ikiwalenga wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu wa Somalia, imezitaka pande zote mbili kuepuka uhasama. Lakini pia Marekani imeonekana kumuunga mkono waziri mkuu Hussein Roble.
Somalia, ambapo hakuna serikali kuu iliyoshikilia kwa upana mamlaka kwa miaka 30 iliyopita, iko katikati kipindi kigumu cha kuandaa uchaguzi, huku kukiwa na makabiliano kati ya Rais Mohamed na waziri mkuu Roble.
Mwezi Aprili, wapiganaji wanaoiunga mkono serikali na wale wa upinzani walipigana katika mitaa ya Mogadishu baada ya Farmajo kuongeza muda wake kusalia madarakani bila uchaguzi mpya.
Soma pia:Rais wa Somalia amuachisha kazi Waziri Mkuu
Wasiwasi wa Marekani
Marekani imesema hatua ya kumsimamisha kazi Waziri Mkuu wa Somalia Mohammed Hussein Roble inatia wasiwasi, na kwamba inaunga mkono juhudi za Waziri Mkuu huyo za kufanyika haraka uchaguzi wa kuaminika nchini humo.
Ofisi ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani inayohusika na masuala ya Afrika iliandika katika mtandao wa Twitter kuwa, Washington iko tayari kuchukua hatua dhidi ya yeyote anayezuia juhudi za Somalia za kupatikana amani.
Mahusiano kati ya Rais Mohamed na waziri mkuu Roble kwa muda mrefu yamekuwa mabaya, lakini matukio ya karibuni yamezusha wasiwasi kwa utulivu wa Somalia wakati nchi hiyo inajitahidi kuandaa uchaguzi uliocholeweshwa muda mrefu na kupambana na uasi wa itikadi kali.