1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikwazo vyaanza kulegezwa Ulaya, New York

12 Mei 2020

Virusi vya corona vimewauwa zaidi ya watu 283,000 kote duniani tangu mripuko kutokea China mwezi Disemba. Zaidi ya visa milioni nne vya maambukizi vimeripotiwa katika nchi 195 duniani.

https://p.dw.com/p/3c3MY
Ukraine Kiew | Coronavirus | Arzt in Schutzanzug
Picha: picture-alliance/NurPhoto/M. Marusenko

Kati ya hao zaidi ya milioni nne walioambukizwa, zaidi ya watu milioni moja na laki tatu wamepona virusi hivyo.

Baadhi ya sehemu za Ulaya na hata mji wa New York huko Marekaniimeanza kulegeza vikwazo taratibu ila ongezeko la maambukizi China na Korea Kusini ni jambo linalomkumbusha kila mmoja kuhusu hatari ya wimbi la pili la maambukizi. Shirika la afya la Duniani WHO limeonya kuhusiana na hatari ya kulegeza vikwazo kwa haraka. Tedros Adhanom Ghebreyesus ni mkurugenzi wa WHO.

"Kuondoa vikwazo ni muhimu kwa kuinua chumi kwa ajili ya kulinda maisha, ila pia ni muhimu kuviangalia kwa jicho la karibu virusi hivi ili hatua za kuvidhibiti ziweze kuchukuliwa endapo kutakuwa na ongezeko la visa," alisema Tedros.

Idadi ya wanaofariki Uhispania imepungua mno

Lakini huku mamilioni ya watu wakiwa wamepoteza ajira zao kutokana na virusi hivyo vya corona na uchumi wa nchi mbalimbali ukiwa umeathirika vibaya, serikali zinataka sana kuharakisha mambo yarudi sawa sawa.

BG Corona-Pandemie Innovationen | Restaurant in Mailand mit Plexiglas
Wateja wakiwa katika mkahawa mjini Milan ItaliaPicha: picture-alliance/dpa/C. Furlan

Nchini Uhispania kama sehemu zengine za Ulaya, maafisa wamepewa moyo na takwimu zinazoonyesha maambukizi na idadi ya vifo kupungua. Uhispania imerekodi vifo 123 katika masaa ishirini na mane yaliyopita huku Italia ambayo ilikuwa kitovu cha virusi hivyo wakati mmoja Ulaya, ikiripoti chini ya wagonjwa elfu moja walio katika vyumba vya wagonjwa mahututi, hiyo ikiwa ndiyo idadi ndogo zaidi tangu Machi 10.

Ufaransa imeshuhudia idadi ya watu wanaofariki kila siku kushuka kwa siku kadhaa ingawa hapo Jumatatu idadi hiyo iliongezeka kwa watu 263. Nchi hiyo imeanza kuibomoa hospitali ya muda ya kijeshi iliyokuwa imejengwa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa mahututi wakati hospitali zilipokuwa zimelemewa na mzigo.

Ujerumani nayo imefuata mkondo wa kulegeza vikwazo kwa baadhi ya majimbo kufungua maduka, mikahawa, shule na sehemu za kufanyia mazoezi ingawa Kansela Angela Merkel ametoa onyo kutokana na takwimu kuonyesha kwamba idadi ya maambukizi inaongezeka tena.

Waliofariki wamepindukia 80,000 Marekani

Huko Uingereza Ligi Kuu ya kandanda nchini humo ambayo ni maarufu sana huenda ikaanza tena Juni mosi baada ya serikali kutoa mwongozo wake kuhusiana na kurudi tena kwa michezo. Waziri Mkuu Boris Johnson amesema anaamini kuwa kurudi kuonyeshwa kwa michezo katika televisheni kutamtia kila mmoja moyo.

Senegal Vereidigung Macky Sall als Präsident
Rais wa Senegal Macky SallPicha: Getty Images/AFP/Seyllou

Lakini nchini Marekani kulingana na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, idadi ya waliofariki imepindukia 80,000 hiyo ikiwa ni idadi ya juu mno kuliko nchi yoyote duniani. Mji wa New York wenye idadi kubwa ya watu ndio ulioathirika sana ingawa gavana wake Andrew Cuomo ametoa ruhusa ya vikwazo kuanza kulegezwa taratibu wiki hii ingawa vikwazo vitaendelea kuwepo katikati ya mji huo hadi angalau mwezi Juni.

Huko Afrika vikwazo vitaanza kulegezwa nchini Senegal huku Rais Macky Sall akisema marufuku ya kutotoka nje usiku yatapunguzwa na misikiti kufunguliwa tena katika nchi hiyo ambayo idadi kubwa ya raia wake ni Waislamu. Huku akithibitisha kwamba vikwazo vitaanza kulegezwa kuanzia Jumanne, Sall amemtaka kila mmoja kuchukua jukumu la kujilinda na kujifunza jinsi ya kuishi vyema na kukabiliana vyema na virusi hivyo kwa wakati huo huo.