1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa nchi za Kiarabu na Kiislam wakutana Saudi Arabia

11 Novemba 2024

Viongozi wa mataifa zaidi ya 50 ya kiarabu na kiislamu wanakutana nchini Saudi Arabia siku ya Jumatatu katika mkutano wa kilele unaotazamiwa kujadili mzozo wa Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/4mrzN
Saudi Arabia | Mkutano wa nchi za kiarabu na Kiislamu mjini Riyadh
Viongozi wa nchi za kiarabu na Kiislamu wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mkutano wao wa kujadili mzozo wa Mashariki ya Kati.Picha: WANA NEWS AGENCY/REUTERS

Kulingana na vyanzo kutoka nchini Saudi Arabia, mkutano huo uliotangazwa mwezi Oktoba, utafanyika katika mji mkuu wa Riyadh na utaangazia kile walichokiita "uchokozi na uvamizi wa Israel dhidi ya maeneo ya Palestina na upanuzi wake hadi nchini Lebanon."

Mwaka mmoja uliopita, Saudi Arabia ilizialika nchi hizo kwenye mkutano kama huo na kamati ya mawaziri mbalimbali iliundwa ili kusimamia mchakato wa kuvimaliza vita vya Gaza, lakini mpango huo hadi sasa haujapata mafanikio yoyote.

Mkutano huo ulizikusanya nchi zilizopo kwenye Jumuiya ya nchi za kiarabu yenye makao yake makuu mjini Cairo na zilizopo kwenye Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu yenye makao yake mjini Jeddah ambapo viongozi walishutumu hatua za majeshi ya Israel huko Gaza na kuzitaja kuwa ni za "kinyama" huku wakishinikiza suluhisho la mataifa mawili.

Ujumbe kwa rais mteule wa Marekani

Donald Trump (kushoto) akiwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Rais mteule wa Marekani Donald Trump (kushoto) akiwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Amos Ben Gershom/IMAGO/ZUMA Press Wire

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema mkutano huo unalenga pia kutoa ujumbe ulio wazi kwa rais mteule wa Marekani Donald Trump kuhusu kile kinachotakiwa na nchi za kiarabu na kiislamu katika suala zima la ushirikiano na Washington kwa kutilia msisitizo kuwa mataifa hayo yanataka mazungumzo, kutuliza mzozo na kukemea harakati za kijeshi za Israel huko  Mashariki ya Kati.

Katika muhula wake wa kwanza, vitendo vya Trump vilimuonyesha wazi kuwa mshirika thabiti wa Israel. Alikaidi makubaliano ya kimataifa kwa kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel na hata kuuhamisha ubalozi wa Marekani hadi eneo hilo.

Vita vyaendelea huku upatanishi ukikwama

Israel inaendesha vita dhidi ya wanamgambo wa Kipalestina wa Hamas katika Ukanda wa Gaza  na wakati huohuo inakabiliana na wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon, na makundi yote hayo yakiungwa mkono na Iran. Mashambulizi ya mwishoni mwa wiki yalisababisha vifo vya makumi ya watu Gaza pamoja na nchini Lebanon.

Mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza
Wapalestina wakishuhudia uharibifu utokanao na mashambulizi ya Israel huko GazaPicha: Omar AL-QATTAA/AFP

Hadi sasa, juhudi za upatanishi zinazosimamiwa na Marekani, Qatar na Misri na zinazolenga kuvimaliza vita hivyo hadi sasa hazijafua dafu. Hivi majuzi Qatar ilitangaza kusitisha ushiriki wake kwenye juhudi za kusaka makubaliano ya kusitisha vita vya Gaza na kuachiliwa kwa mateka na hivyo kuzusha wasiwasi zaidi.

Lakini baadaye wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo ilikanusha taarifa zilizosambazwa kwamba serikali mjini Doha ilitaka ofisi ya Hamas nchini humo kufungwa kutokana na kutotimiza majukumu ya kuanzishwa kwake.

Soma pia: Qatar yajiondowa upatanishi vita vya Gaza

Ahmed Al-Borsh ni Mpalestina anayeishi katika kambi ya Jabalia:

" Tunaitaka Qatar iendeleze juhudi zake za kukomesha vita hivi ambavyo vimeathiri nyanja zote na kuyageuza maisha ya Wapalestina kuwa jehanamu isiyoweza kuvumilika. Kwa hivyo, matumaini yangu ni kwamba Qatar itaendeleza juhudi zake, kwa sababu ndiyo iliyo karibu zaidi na watu wa Palestina."

Hata hivyo, serikali mjini Doha imesema inaweza kurejea kwenye juhudi za upatanishi ikiwa pande zote mbili zitadhihirisha nia njema na utashi wa kisiasa wa kuumaliza mzozo huo.

(Vyanzo: AFP, DPAE, AP)