Vita vyaendelea Gaza, mchakato wa mazungumzo wakwama
25 Julai 2024Israel imeendeleza mashambulizi huko Gaza na kuwaamuru maelfu ya Wapalestina kuondoka maeneo ya kusini mwa ukanda huo hasa katika mji wa Khan Younis. Raia walitekeleza amri hiyo ya kuondoka sasa wanaishi katika mazingira duni huku wengine wakilala nje.
Wizara ya afya huko Gaza inayodhibitiwa na Hamas imesema pia kuwa zaidi ya Wapalestina 39,100 wameuawa katika vita hivyo vilivyoanza Oktoba 7 mwaka jana. Jeshi la Israel limetangaza pia kuwa limefanikiwa kuipata miili ya mateka watano kutoka huko Gaza.
Soma pia: Amnesty: Israel ikomeshe mateso kwa Wapalestina Gaza
Ama katika hatua nyingine, maafisa kutoka Misri, Israel, Marekani na Qatar walitarajiwa kukutana hivi leo mjini Doha kwa lengo la kuanzisha upya mazungumzo ya kusitisha mapigano ili kuvimaliza vita kati ya Israel na Hamas na kuwakomboa mateka waliosalia. Lakini afisa wa Israel amesema kwamba wajumbe wa Israel walichelewa kuwasili nchini Qatar lakini akasema kuna uwezekano wa ujumbe huo kutumwa wiki ijayo.
Netanyahu alihutubia Bunge la Marekani
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alilihutubia siku ya Alhamisi Bunge la Marekani na kuapa kuendeleza vita dhidi ya kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Katika hotuba yake kwenye Bunge la Marekani iliyonuia kutafuta uungwaji mkono katika vita vya Gaza, Netanyahu amewaambia wabunge kuwa maadui wa Israel ni maadui pia wa Marekani huku akiapa kuwa ataendeleza vita vita hivyo hadi atakapolitokomeza kabisa kundi la Hamas:
"Siku tutakapoishinda Hamas, ndipo Gaza mpya itakapoweza kuzaliwa. Maono yangu kwa siku hiyo ni ya Gaza isiyo na wanamgambo wala watu wenye misimamo mikali. Israel haitaki kuidhibiti tena Gaza, lakini kwa siku zijazo, ni lazima tuwe na udhibiti mkubwa wa usalama eneo hilo ili kuzuia kuibuka tena kwa ugaidi, ili kuhakikisha kwamba Gaza haiwi tena tishio kwa Israel."
Alipokuwa akitoa hotuba iliyodumu kwa karibu saa nzima, Netanyahu alishangiliwa na wabunge wengi wa Republican lakini wabunge kadhaa wa chama cha Democratic walisusia hotuba hiyo kutokana na matendo ya Israel katika vita hivyo.
Pia mamia ya waandamanaji walikusanyika nje ya Bunge kulaani ujio wa Netanyahu huku wakiwa na mabango yaliyosomeka: "Netanyahu ni mhalifu wa kivita."
Waziri Mkuu huyo wa Israel amewashtumu waandamanaji hao wanayoiunga mkono Palestina na kuwaita "wajinga wenye manufaa" wanaopokea ufadhili wa siri kutoka kwa Iran. Netanyahu anatarajiwa hivi leo kukutana kwa mazungumzo na rais Joe Biden na mgombea urais Kamala Harris na baadaye kesho atakutana pia na Donald Trump.
(Vyanzo: Mashirika)