1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waangalizi: Israel yashambulia Syria na kuua wapiganaji 8

25 Novemba 2020

Jeshi la Syria limesema Israel imeanzisha mashambulio ya angani eneo la kusini nje kidogo ya mji wa Damascus kunakoaminiwa kuwa na wanajeshi wengi wa Iran. Hili ni shambulio la pili kufanyika ndani ya wiki moja.

https://p.dw.com/p/3lnXk
Syrien Symbolbild Ras al-Ain
Picha: picture-alliance/Photoshot

Kulingana na taarifa kutoka kwa jeshi hilo la Syria, shambulio la angani kutoka Israel katika eneo la kimkakati ambalo Israel ililishambulia awali lilivurumishwa kutoka eneo la milima ya Golan na kusababisha uharibifu wa mali.

Wanajeshi walioasi wamesema shambulio hilo lililenga kambi ya kijeshi katika eneo la Jabal Mane karibu na mji wa Kiswa kuliko jeshi la Iran takriban kilomita 15 kutoka Kusini mwa mji wa Damascus.

Kwa upande wake shirika la uangalizi la haki za binaadamu nchini Syria, limesema shambulio hilo la angani limesababisha mauaji ya wapiganaji wanane wanaoliunga mkono jeshi la Iran.

Soma pia: Jeshi la Israel lakiri kuwashambulia washukiwa wa wanamgambo Syria

Shirika hilo limeongeza kuwa shambulio lililenga bohari ya silaha kusini mwa Syria inayoshikiliwa na wanajeshi wa Iran na washirika wao wa Hezbollah. Hata hivyo uraia wa wapiganaji waliouwawa hadi sasa haujajulikana.

Wakati huo huo, shirika la habari ya Syria, SANA limeripoti shambulio jengine katika kijiji cha Rwihinah kusini mwa mkoa wa Quneitra karibu na maeneo yanayokaliwa ya milima ya Golan bila ya kuripoti majeruhi wowote katika shambulio hilo.

Shirika la habari la SANA lilisema shambulizi hilo lilisababisha mauaji ya wanajeshi watatu wa Syria.
Shirika la habari la SANA lilisema shambulizi hilo lilisababisha mauaji ya wanajeshi watatu wa Syria.Picha: picture-alliance/dpa/J. Hollander

Jeshi la Israel limekataa hadi sasa kutoa tamko lolote juu ya shambulio la leo lilipotafutwa kufanya hivyo na shirika la habari la AFP. Israel imeshawahi kutekeleza mashambulizi ya angani na mashambulizi pia ya makombora nchini Syria, ikivilenga vikosi vya serikali pamoja na vikosi vya Iran na kundi la Hezbollah kutoka Lebanon wanaouunga mkono utawala wa rais wa Syria, Bashar al Assad.

Soma pia: Israel yafanya mashambulizi "makubwa" Syria

Wiki iliyopita, ndege za kivita za Israel zilishambulia ngome za Iran nchini Syria kwa kile jeshi la Israel ilichokiita majibu ya kulipiza kisasi kwa kile ilichosema ni mabomu yaliopatikana karibu na kambi zake katika milima ya Golan.

Shirika la habari la SANA lilisema shambulizi hilo lilisababisha mauaji ya wanajeshi watatu wa Syria, huku wapiganaji saba wa kigeni waliuwawa. Vita vya Syria ambavyo mpaka sasa vimesababisha mauaji ya watu 380,000 vimesababisha mamilioni pia kukosa makaazi yao tangu vilipoanza mwaka wa 2011 kwa maandamano makubwa ya kuipinga serikali.