Waasi wa Tigray wapuuza usitishaji wa vita wa Ethiopia
29 Juni 2021Tangazo hilo la TPLF la kukaidi hatua ya serikali ya kusitisha mapigano limekuja usiku wa kuamkia leo, muda mfupi baada ya wapiganaji wa chama hicho kusema wamechukua udhibiti wa mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekele. Kabla ya hapo, serikali ya shirikisho la Ethiopia inayoongozwa na waziri mkuu Abiy Ahmed ilikuwa imechukuwa maamuzi ya upande mmoja ya kusitisha mapigano.
Soma zaidi: Ethiopia: Mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekele washambuliwa vikali
Katika tangazo hilo la TPLF, chama hicho ambacho kinachukuliwa na serikali kuu kama cha uasi kitafanya kila linalowezekana kuhakikisha ukombozi na usalama wa watu wa jimbo la Tigray. Getachew Reda, msemaji wa chama hicho, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa lengo la adui wanayepigana naye ni kulibana jimbo la Tigray na kuhakikisha kuwa watu wake wanasalimu amri, na kuapa kuwa hilo halitowezekana.
Hamasa miongoni mwa wapiganaji wa TPLF
Katika mazingira hayo ya mafanikio, mmoja wa wapiganaji wa tawi la kijeshi la TPLF, Teheras Tsega Berhan amesema wapiganaji wao wana ari kubwa ya mapambano.
''Vijana wamejawa na hamasa na wanamiminika katika vituo vya mafunzo, kujiunga na mapambano. Adui yetu anazidi kudhoofika, na anashindwa,'' amesema Berhan.
Vita vya Tigray vimekuwa vikiendelea kwa karibu miezi minane, na kwa muda mrefu wapiganaji wa TPLF na viongozi wao walikuwa wanajichimbia vichakani bila kupiga hatua yoyote kubwa.
Soma zaidi: Waethiopia washiriki uchaguzi ambao ni mtihani kwa Abiy Ahmed
Lakini wiki iliyopita walianzisha mashambulizi makali wakati serikali ya Addis Ababa ikifanya uchaguzi katika majimbo mengine isipokuwa Tigray.
Addis Ababa yasisitiza 'inapambana na wahalifu'
Matokeo ya uchaguzi huo bado hayajatangazwa lakini yanatarajiwa kumpa ushindi waziri mkuu Abiy na vyama vinavyomuunga mkono.
Msemaji wa TPLF anadai kuwa kabla ya muda mrefu watakuwa wamemaliza kazi ya kulifurusha jeshi la Ethiopia kutoka jimboni mwao, ili wakaazi wa jimbo hilo waweze kufanya kazi zao kama kawaida.
Soma zaidi: Ethiopia: Amnesty yadai 'mauaji ya wengi' yamefanyika Tigray
Serikali kuu ya mjini Addis Ababa haijatoa tamko kuhusu taarifa ya TPLF kuukamata mji wa Makele, na msemaji wake Dina Mufti hata anakanusha kuwepo kwa vita, akisema kinachoendelea ni kupambana na wahalifu.
''Hatusemi kuna vita, tunasema kuna operesheni ya kuhakikisha sheria inaheshimiwa. Mtu anapokiuka sheria ya nchi lazima awajibishwe.''
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema amezungumza na pande mbili katika vita hivyo, na kuzikumbusha kuwa hali iliyopo ni ushahidi mwingine kuwa mizozo haisuluhishwi kwa mtutu wa bunduki.
afpe, ape