1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachambuzi: Watanzania walitarajia utenguzi wa Nape

22 Julai 2024

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amewafuta kazi mawaziri kadhaa ikiwemo waziri wa mambo ya nje, January Makamba na waziri wa habari Nape Nnauye ambaye alitoa matamshi yaliotafsiriwa kuwa na utata hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/4iaQG
Dar es salaam, Tanzania | Rais Samia Suluhu Samia Suluhu Hassan
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Samia Suluhu HassanPicha: AP Photo/picture alliance

 Katika tangazo la ghafla lililotolewa jana usiku na ikulu, Rais pia amefanya mabadiliko katika maeneo mengine ikiwemo kuwahamisha nyadhifa mawaziri wake. 

Kumekuwa na maoni mchanganyiko yanayoendelea kuibuka kuhusiana na hatua ya Rais Samia kuwapiga kalamu nyekundu watendaji wake hasa hatua yake ya kusafisha kabisa wizara ya mambo ya nje ambayo waziri Makamba na manaibu wake wote wawili kuondoka katika wizara hiyo.

Mjadala unashika kasi ni kwa nini mawaziri hao vijana, Makamba na Nape wameondolewa wakati huu na hasa kukiwa na vuguvugu kubwa linaloendelea kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwa huu na ule mkuu wa hapo mwakani ambako chama tawala CCM kimekuwa kikijaribu kuhubiri chaguzi hizo zitafanyika katiika mazingira ya haki na kweli.

Soma pia:Nape akosolewa kwa matamshi yake ya njia za kushinda uchaguzi

Ingawa taarifa ya ikulu haijaeleza sababu za kuenguliwa kwa watendaji hao, hata hivyo baadhi ya wafuatiliaji wa siasa za Tanzania wanajaribu kuchora ramani ya matukio yanayowagusa wanasiasa hao ikiwemo ile inayohusu moja kwa moja ushawishi wao ndani ya chama.

Nape hivi karibuni aliingia katika ukosoaji mkubwa kutokana na kauli yake ya udanganyifu katika kura.

Wachambuzi: Utenguzi huu ulitarajiwa na wengi

Baadhi ya wachambuzi na wafuatiliaji wa mambo kwenye mitandao wanaojadili mabadiliko hayo ya mawaziri wamekuwa na mitazamo inayoelekea kufananisha hatua hiyo huku wengine wakisema lilikuwa ni suala la kusubiri wakati tu. 

Mchambuzi Joseph Mwanzi anasema kwa kufanya mabadiliko hayo huenda Rais Samia anatembea katika kauli zake za kutaka mabadiliko ya kweli

Paul Makonda nje, aingia Aboubakari Kunenge, mkuu mpya wa Dar Es Salaam

Gilbert Mgube ambaye kwa muda mrefu amekuwa akizifuatilia siasa za Tanzania anasema ili kujenga  mustakabali mwema wa maridhiano ya kitaifa, wanasiasa wanapaswa kubeba dhambi zao pindi wanapokengeuka.

Soma pia:CCM yawaonya makada wake kuelekea mbio za uchaguzi

Makamba na Nape wamekuwa wakitembea katika hali ya kupanda na kushuka katika medani ya siasa za Tanzania na kwamba wakati mmoja walipotea kabisa katika ramani za siasa.

Walishika alama za juu wakati wa utawala wa awamu ya tano wa Rais Hayati John Magufuli lakini baadaye aliwafuta kazi kabla ya kurejeshwa na Samia ambaye naye sasa amewafuta kazi pia.

Ama, katika mabadiliko hayo mapya, Rais Samia amemteua balozi aliyekuwa Italia Mahmoud Thabit Kombo kuwa waziri mpya wa mambo ya nje, wakati aliyekuwa waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, Jerry Silaa amepelekwa wizara ya habari, mawasiliano na teknolojia na nafasi yake kuchukuliwa na Degratius Ndejembi.