Wafungwa wa kwanza wa Kipalestina waachiliwa
14 Agosti 2013Mji wa Ramallah uko kwenye furaha siku ya leo, kwani maelfu ya watu wamejitokeza kuwalaki wafungwa hao wa Kipalestina, ambao Israel imesema inawaachia kama bishara ya nia yake njema ya kuyaendeleza mazungumzo ya amani.
"Siwezi hata kuzielezea hisia zangu kwa maneno. Kwa hakika nina furaha kubwa sana, kwa sababu hili ni jambo nililolingojea kwa muda mrefu - ingawa kwa upande mwengine, bado kuna waume zetu wengine wengi kwenye jela za Israel. Tunaomba nao pia waachiliwe huru hivi karibuni." Amesema Fatima Irsheid, ambaye mumewe, Yussuf, ni miongoni mwa wafungwa waliopewa msamaha huo.
Hii ni awamu ya kwanza ya kuwaachia wafungwa 104, ambao wengi wao walikuwa wanatumikia vifungo vya maisha nchini Israel kwa makosa makubwa yakiwemo ya mauaji.
Israel yaapa kutanua makaazi ya walowezi
Lakini wakati Israel ikiita hii kuwa ni ishara njema ya kukunjua mkono wa mazungumzo, kwa upande mwengine Waziri wa Nyumba wa nchi hiyo, Uri Ariel, ameapa kwamba atajenga maelfu ya nyumba za walowezi kwenye Ukingo wa Magharibi.
"Tutajenga maelfu ya nyumba ndani ya mwaka ujao kwenye Judaea na Samaria. Na hakuna wa kutuambia wapi tunaweza kujenga," alisema waziri huyo akitumia majina yaliyomo kwenye Biblia kuutaja Ukingo wa Magharibi kupitia tangazo lake lilitolewa na redio ya serikali.
Ariel ni kiongozi namba mbili wa chama chenye siasa kali za Kiyahudi, Jewish Home Party, kinachopingana na uanzishwaji wa dola ya Palestina, na pia ni miongoni mwa wajumbe wa baraza la mawaziri na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, waliopinga vikali hatua ya kuachiliwa huru kwa wafungwa wa Kipalestina. Ariel ameuita ujenzi huo kuwa ni "mwanzo tu", na kwamba nyumba zaidi zitajengwa.
Mashaka ya kufanyika kwa mazungumzo
Kauli yake iliyotafsiriwa kama ya uchokozi inakuwa huku timu za mazungumzo kutoka pande zote mbili zikiwa kwenye matayarisho ya mwisho mwisho, kabla ya kuingia kwenye vikao vyao vya mwanzo, kufuatia juhudi za Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry.
Hata hivyo, Waziri wa Nyumba wa Israel, Uri Ariel, hajasema kitu kipya sana, zaidi ya kufafanua msimamo uliotangazwa na nchi yake siku tatu nyuma, pale baraza la mawaziri lilipobainisha mpango wake wa kuendelea na ujenzi wa nyumba mpya 2,129, zaidi ya nusu na robo yake zikiwa kwenye eneo la Jerusalem ya Mashariki.
Awali, siku ya Jumapili, baraza hilo lilitoa orodha ya ujenzi wa nyumba 1,187 mpya, lakini punde baadaye ikaongeza nyengine 942, jambo ambalo limewakasirisha sana Wapalestina, ambao wanalichukulia eneo la Jerusalem ya Mashariki kuwa mji mkuu wa taifa lao lijalo.
Yasser Abdi-Rabbo, afisa wa ngazi za juu wa chama cha ukombozi cha Palestina, PLO, ameliambia shirika la habari la AFP, kwamba hatua hiyo ya Israel inatishia kuyatoa roho mazungumzo ambayo bado yangali tumboni.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo