Israel na Palestina zahimizwa kuchukulia mazungumzo ya amani kwa uzingativu
13 Agosti 2013Huku awamu mpya ya mchakato wa kufufua mazungumzo ya amani yakiwa katika kiwango cha awali, baada ya kukwama kwa miaka mitatu, kuidhinishwa kwa ujenzi wa makaazi mapya 1,200 mashariki mwa Jerusalem na kwingineko katika Ukingo wa Magharibi kumewaghadhabisha mno Wapalestina.
Mpango huo wa ujenzi ulifuatiwa haraka na tangazo la Israel la kuwaachilia huru wafungwa 26 wa Kipalestina kabla ya kuanza kwa mazungumzo kati yao hapo kesho mjini Jerusalem na kuonyesha mtindo wa kuuma na kuvungia unaotumiwa na Israel.
Kuachiliwa kwa wafungwa hao 26 ni sehemu ya mpango ya kuwaachilia wafungwa 104 kwa jumla katika awamu nne kulingana na hatua zitakazopigwa katika mazungumzo hayo kati ya Israel na Palestina. Mkuu wa ujumbe wa Palestina kwenye mazungumzo hayo, Saeb Erekat, amesisititza umuhimu wa kuachiliwa kwa wafungwa ili kuendeleza mazungumzo.
Vuta nikuvute kabla ya mazungumzo
Huku baadhi ya mawaziri wa Israel wakikosoa kuachiliwa kwa wafungwa hao, maafisa wa Palestina wameukosoa mpango huo wa ujenzi ambao pia Marekani na Umoja wa Ulaya hapo jana zilisema sio halali na unatishia kusambaratisha juhudi za kurejea katika meza ya mazungumzo.
Duru ya mwisho ya mazungumzo yalisambaratika mwaka 2010 kutokana na suala kama hilo hilo la ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika eneo linalozozaniwa na pande hizo mbili.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, akiwa ziarani Colombia hapo jana alijaribu kutuliza ghadhabu zilizozuka kabla ya mazungumzo hayo muhimu, kwa kusema kuwa kwa kiasi fulani mpango huo wa ujenzi ulikuwa unatarajiwa na badala kuzitaka pande zote mbili kutatua matatizo yao makuu.
Ujenzi usiwe kichocheo cha kusambaratisha mazungumzo
Kerry, ambaye ndiye mpatanishi mkuu kati ya Israel na Palestina, amesema hatarajii tangazo hilo la mwishoni mwa wiki iliyopita la Israel kuwa kizingiti dhidi ya mazungumzo hayo na kusisitiza kuwa Marekani inachukulia ujenzi huo kutokuwa halali.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje amesema ameweka miadi kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, aliyefanyiwa upasuaji siku chache zilizopita na anatarajia kuzungumza naye ili kutatua mzozo huo.
Kuachiliwa kwa wafungwa kumezikasirisha familia za waliouawa na wafungwa hao nchini Israel na ripoti za mashirika ya habari ya Mashariki ya Kati zimedokeza kuwa tangazo la ujenzi wa nyumba za walowezi lilinuia kuwafurahisha washirika wa Netanyahu serikalini waliopinga kuachiliwa kwa wa wafungwa hao.
Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef