Wapalestina, Waisraili bado hawaaminiani
30 Julai 2013Wakati hapo jana Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, akimtangaza balozi wa zamani wa nchi hiyo kwa Israel, Martin Indyk, kuwa mjumbe maalum wa Marekani kwenye mazungumzo kati ya Israel na Palestina, matarajio ya raia wa kawaida wa pande hizo mbili si makubwa.
Mara kadhaa pia mazungumzo kama haya yameanzishwa, matumaini yakajengwa na suluhisho likaaminiwa, lakini punde huporomoka na kila jambo likaanza tena mwanzo. Ndivyo asemavyo Marcus Gad, mwanafunzi wa Kiisraeli aliyekulia nchini Uswisi.
“Ni bora kuwanayo kuliko kutokuwanayo kabisa, lakini mambo hayawezi kuwa mabaya zaidi ya hapo na hayawezi kuendelea kuwa kama yalivyo. Lakini matumaini yangu siyaweki kwa Bibi Netanyahu. Na sijui ikiwa kweli Wapalestina wanataka amani.” Amesema Gad.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na gazeti la kila siku la Haaretz nchini Israel, asilimia 55 ya 3watu watapigia kura makubaliano na Wapalestina, lakini asilimia 70 wanashuku ikiwa kweli kutakuwa na makubaliano yatakayofikiwa baina ya pande hizo mbili.
Imani ya Wapalestina iko chini zaidi
Upande wa Palestina matarajio ni ya chini zaidi, kwani asilimia 69 hawaamini kutelekezwa kwa suluhisho la dola mbili huru ndani ya miaka mitano ijayo. Imad Munad, muuza vitabu wa Kipalestina anayeishi Jerusalem ya Mashariki, licha ya kujichukulia mwenyewe kuwa ni mtu mwenye matumaini, lakini linapokuja suala la “mazungumzo ya amani”, yeye pia ana shaka zake.
“Hata kama watu wengi wanazungumzia juu ya mchakato wa amani, lakini watu hapa hawana imani nao. Kimaumbile mimi ni mtu mwenye matumaini, lakini tangu mwaka 1994, kwa miaka 20 sasa, na kabla ya hapo huko Madrid, tumekuwa tukiujaribu kupatana na Israel, na sasa kwa ukweli kabisa, sina matumaini makubwa kwamba kuna chochote kitakachopatikana.” Amesema Munad.
Moja ya vikwazo vya mwisho katika kurejelewa kwa mazungumzo kiliondoshwa siku ya Jumapili, pale baraza la mawaziri la Israel lilipoidhinisha kuachiwa huru kwa wafungwa 104 wa Kipalestina.
Waisraili wapingana na Netanyahu
Lakini hatua hii iliyokusudiwa kuwa ishara ya dhamira njema ya kisiasa haikuja kwa urahisi. Ilikuwa ni baada tu ya masaa kadhaa ya mijadala kwenye baraza hilo la mawaziri, ndipo hatimaye Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akaweza kupata kura 13 za wajumbe wa baraza lake kuunga mkono hatua hiyo, huku saba wakipinga na wawili wakijiepusha kupiga kura.
Wafungwa hao 104, wote walikamatwa kwa tuhuma za ugaidi kabla ya kusainiwa kwa Mkataba wa Oslo wa mwaka 1993. Baadhi yao walikuwa hata wamefungwa maisha kwa sababu waliwaua raia wa Israel.
Uamuzi huu ulikuwa mgumu sana kwa Waisraili wengi, anasema muuza duka Elizier Matoug, aliye Jerusalem ya Magharibi, akiongeza kwamba “Hili ni kosa kubwa, tunawaachia huru wauwaji wote hawa, na hatupati chochote. Hili halikupaswa kufanyika na litakuwa na matokeo mabaya.”
Lakini kwa ujumla, licha ya kuvunjika kwao moyo, sauti kutoka pande zote mbili zingelipenda kuona mazungumzo haya ya Washington yakifanikiwa.
Wasiwasi wao ni kuwa nayo yasije yakawa mazungumzo ya kufufua mazungumzo, kisha yakafa tena na kuja mazungumzo ya kufufua mazungumzo ya kufufua mazungumzo. Mduara wa papo kwa papo, ambao hauna faida kwa yeyote.
Mwandishi: Talia Krämer
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo