1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakulima waanza maandamano Ujerumani

9 Januari 2024

Wakulima nchini Ujerumani wamezuia barabara na kukwamisha shughuli za umma kwa kutumia matrekta leo, wakianza mgomo wa nchi nzima utakaodumu kwa wiki moja kupinga kuondolewa kwa ruzuku ya kilimo

https://p.dw.com/p/4azIc
Lango la Brandenburg - maandamano ya wakulima wa Ujerumani kupinga ruzuku ya ushuru wa magari kwa serikali inayoitwa muungano wa Ampel ya Ujerumani mbele ya Lango la Brandenburg huko Berlin, Ujerumani Januari 8, 2024.
Wakulima wa Ujerumani walioandamana kupinga ruzuku ya ushuru wa magari kwa serikali mjini Berlin, Ujerumani Januari 8, 2024.Picha: Nadja Wohlleben/REUTERS

Wakulima hao wakiwa kwenye misafara ya matrekta na malori, baadhi yakiwa yamepambwa na mabango yenye ujumbe usemao, "hakuna bia bila wakulima" pamoja na mabango ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD, wameanza maandamano tangu alfajiri ya leo, na kuwafanya wafanyakazi katika baadhi ya mashirika kufika kwenye vituo vya kazi kuchelewa. Mjini Berlin, msururu wa matrekta ulizuwia njia kuu inayoelekea lango maarufu la Brandenburg.

Polisiimesema barabara za kawaida na njia za kuunganisha barabara kuu zimezuiwa katika maeneo mengi nchini humo, ikiwemo vivuko kadhaa vya mpakani na Ufaransa, na kusababisha msongamano wa magari wakati wa saa za asubuhi ambapo watu wengi wanaelekea kazini.

Soma zaidiWakulima wa Ujerumani wauzingira mji Berlin katika mgomo wa trekta

Wakulima wanasema mipango ya serikali ya kusitisha nafuu ya kodi, ambayo inawasaidia kuokoa jumla ya yuro milioni 900 kwa mwaka, itawafanya washindwe kuendelea na biashara.

Reinhard Jung ni msemaji wa chama chawakulima huru amesema wameandamana kupinga ongezeko la kodi, huku wakiita kodi hizo ni za dhuluma, lakini pia amesema wanataka mabadiliko ya mwelekeo katika sera ya kilimo. ''Namna mambo yalivyokwenda katika miaka mitano, sita, saba iliyopita, hata kabla ya serikali ya sasa, haiwezi kuendelea. Tunahitaji sera inayoipa sekta ya kilimo umuhimu wake katika jamii na kutambua kwamba tasnia yetu ina haki ya kuwepo''.

Pichani ni  matrekta yakiwa yapangwa foleni, huku wakulima wa Ujerumani wakishiriki katika maandamano ya kupinga kukatwa kwa ruzuku ya ushuru wa magari, huko Taufkirchen karibu na Munich, Ujerumani, Januari 8, 2024.
Matrekta yakiwa yamepangwa katika foleni kufuatia maandamano ya wakulima kupinga ruzuku ya ushuru wa magari, nchini UjerumaniPicha: LEONHARD SIMON/REUTERS

Serikali kuu ya Ujerumani inayoongozwa na vyama vitatu, ililaazimika kutafuta namna ya kufidia  pengo la  mabilioni ya yuro katika bajeti yake ya mwaka huu baada ya hukumu ya mahakama mwezi Novemba kuvuruga mipango yake ya matumizi. 

Mahakama ya katiba yaitaka serikali ibatilishe uamuzi wake

Katika hukumu hiyo ya mahakama ya katiba, serikali ilipigwa marufuku kutumia kinyume na mipango, kiasi cha yuro bilioni 60 zilizosalia kwenye fedha za mkopo wa ufufuaji uchumi kutokana na athari za janga la Uviko-19, hali iliyosababisha mzozo wa kibajeti. Wakulima wanasema wametwikwa mzigo wa makato hayo ya bajeti isivyo haki, na wameapa kuzuwia njia kuu ya usafiri kwa wiki nzima mpaka serikali itakaposikiliza kilio chao.

Soma zaidi: Mahakama Kenya yatulipilia mbali kesi dhidi ya mazao ya GMO

Uchunguzi wa maoni ya wananchi uliofanywa na kituo cha televisheni ya umma cha NTV, umeonyesha uungwaji mkono mkubwa wa umma, ambapo asilimia 91 ya waliohojiwa wamesema maandamano hayo ya wakulima yalikuwa na msingi. Hata hivyo Naibu wa Kansela ambaye pia ni waziri wa uchumi Robert Habeck, ameelezea wasiwasi kwamba maandamano hayo yanavamiwa na wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia.

Mwenyekiti wa chama cha Wakulima wa UjerumaniDVB, pia ameelezea wasiwasi kwamba maandamano hayo yanatumiwa na wanaharakati wa chama cha siasa kali cha Afd kwa ajili ya kueneza ajenda zake, baada ya chama hicho kuhanikiza zaidi kwenye maandamano hayo huku msemaji wake akitumia fursa hiyo kuikosoa serikali na kusema chama chao kiko tayari kuchukuwa majukumu kwa maslahi ya wananchi.