1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

Ujerumani na Ufaransa zahimiza uwajibikaji Ethiopia

13 Januari 2023

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock na mwenzake wa Ufaransa, Catherine Colonna wamesema maridhiano hayawezi kufikiwa bila kuwepo haki, na kulaani ubakaji unaofanywa kwenye vita vya Ethiopia na Ukraine.

https://p.dw.com/p/4M7WR
Äthiopien Annalena Baerbock zu Besuch
Picha: Fana Broadcasting Corporate S.C.

Ziara ya Bearbock na Colonna ilianza siku moja baada ya waasi wa Tigray kutangaza wanaanza kusalimisha silaha zao za kivita kwa serikali ya Ethiopia. Wanadiplomasia hao ambao wanaizuru Ethiopia katika juhudi za kuunga mkono mkataba wa amani uliosainiwa Novemba, mwaka uliopita, wamesema wanaunga mkono maendeleo mazuri ambayo wanahimiza yaendelee katika mchakato wa amani kati ya serikali ya Ethiopia na Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF. Waasi wa Tigray waanza kuzisalimisha silaha zao nzito

Wakizungumza jana baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, mawaziri hao wametoa wito wa kuanzishwa kwa utaratibu wa mpito utakaosimamia haki ili kuhakikisha waliohusika na ukiukaji wa haki za binaadamu wanashtakiwa.

Baerbock amesema suala la uwajibikaji ni muhimu sana kwa ajili ya mustakabali wa Ethiopia na mchakato wa amani, lakini pia kuelekea katika kuimarisha sheria za kimataifa. "Sisi Wajerumani na Wafaransa tunalijua hili kutokana na uzoefu wetu wenyewe, kwamba maridhiano hayawezi kupatikana mara moja. Lakini bila matarajio ya kuwepo haki kwa waathirika wa uhalifu, maridhiano na amani ya kudumu havitafanikiwa," aliongeza Baerbock.

Annalena Baerbock in Äthiopien
Wanadiplomasia wa Ujerumani na Ufaransa katika picha ya pamoja waziri mkuu wa EthiopiaPicha: Florian Gärtner/imago images/photothek

Kwa upande wake Waziri Colonna amesema uhasama umemalizika, msaada umeanza kufika kwenye majimbo ambayo yalikuwa hayajapokea misaada na waasi wameanza kukabidhi silaha.

"Niamini mimi, kama alivyosema Annalena, ninafahamu ujasiri mliochukua, pande zote za serikali ya shirikisho na viongozi wa Tigray, kuchagua amani. Kwani inahitaji ujasiri na hata maono kuchukua uamuzi kama huo."

Kwa mujibu wa wanadiplomasia hao wa Ujerumani na Ufaransa, sheria za kimataifa ziko wazi: kulindwa kwa raia ndiyo kipaumbele cha kwanza katika mizozo, na ubakaji ni uhalifu wa kivita. Bearbock amesema katika mzozo wowote ule, walioko hatarini zaidi ni watu wasio na hatia, watoto wengi, pamoja na wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada ambao wamekuwa wakilengwa wakati wanajaribu kuwahudumia wanawake, watoto na wagonjwa.Wanajeshi wa Eritrea waondoka kaskazini wa Ethiopia

Mawaziri hao wameitaka serikali ya Ethiopia kuendelea kufuata njia ya amani na kwamba Umoja wa Ulaya, lakini hasa Ujerumani na Ufaransa wanataka kusaidia katika kulijenga hilo.

Jana mawaziri hao walilitembelea ghala kubwa la nafaka la Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, lililoko nje ya mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, ambako nafaka zinazotoka Ukraine zinahifadhiwa.

Wakiwa katika ghala hilo, Baerbock alimkosoa Rais wa Urusi, Vladmir Putin kwa kuuzidisha mzozo wa chakula ulimwenguni. Amesema Putin anatumia nafaka na chakula kama silaha, hatua inayozidisha hali mbaya ya upatikanaji wa chakula ulimwenguni kote, kwani ukame pia umeendelea kuongezeka duniani kote.

Mawaziri hao wawili leo Ijumaa wanatarajiwa kukutana kwa mazungumzo na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat.