Wapatanishi wa Palestina wajiuzulu
14 Novemba 2013Viongozi waliowasilisha barua za kujiuzulu ni pamoja na mpatanishi mkuu Saeb Erakat na Mohammed Shtayyeh, hatua walioichukua baada ya Waziri wa Makaazi na Ujenzi wa Israel, Uri Ariel kutangaza kuendeleza ujenzi wa nyumba zipatazo 24,000 kwenye Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki.
Hata hivyo mpango huo mpya ulikosolewa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na alimuamuru Waziri Ariel kuusitisha akisema kuwa utasababisha mvutano usio wa lazima na jumuiya ya kimataifa.
Afisa wa chama cha ukombozi wa Wapalestina-PLO, Xavier Abu Eid amesema Erakat na Shtayyeh waliwasilisha barua zao kwa Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, kabla ya Netanyahu hajasitisha ujenzi huo. Netanyahu amesema waziri wake alifanya maamuzi hayo peke yake bila kumshirikisha.
Abbas na Kerry wazungumza kwa simu
Jana Jumatano (13.11.2013) Abbas alizungumza kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry anayesimamia mazungumzo hayo kwa kiasi kikubwa, na akamuhakikishia nia yake ya kutaka kuendelea kwa mazungumzo hayo. Abbas amesema mazungumzo yataendelea hata kama ujumbe wa wapatanishi wa Palestina umejiondoa.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Misri cha CBC, Abbas amesema wanajaribu kuwashawishi wapatanishi hao kurejea kwenye mazungumzo hayo ya amani, ama watachagua wapatanishi wapya. Hata hivyo, bado haijafahamika wazi iwapo Abbas atakubali barua hizo za kujiuzulu, hadi hapo atakapokubali kusaini.
Afisa mwandamizi wa PLO, Hanan Ashrawi amesema iwapo hatua ya kujiuzulu wapatanishi hao itakuwa rasmi, itakuwa vigumu kwa Abbas kutafuta wapatanishi wengine, kwa sababu hakuna mtu ambaye anataka kujihusisha katika mchakato wa amani ambao mwelekeo wake haueleweki.
Israel ilitangaza mpango wa ujenzi wa makaazi mwezi uliopita
Mwezi uliopita Ariel alitangaza zabuni kwa mpango wa kujenga kiasi nyumba 20,000 katika Ukingo wa Magharibi na nyumba 4,000 Jerusalem Mashariki, bila kushauriana na Netanyahu.
Kutangazwa kwa zabuni hizo ni hatua za awali za mchakato wa ujenzi. Netanyahu amesema mvutano kuhusu ujenzi wa makaazi ya walowezi unatishia kudhoofisha kampeni dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran. Palestina inalichukulia eneo la Ukingo wa Magharibi kama taifa lake la baadaye.
Waziri wa Nishati wa Israel, Silvan Shalom jana ameweka bayana kwamba nchi hiyo itaendelea na ujenzi wa makaazi ya walowezi, huku ikiwa makini katika suala la kuutangaza mpango huo katika siku za usoni. Katika ziara yake ya Mashariki ya Kati hivi karibuni, Kerry aliitolea wito Israel kuweka mpaka katika kazi ya ujenzi wa makaazi ya walowezi, ili kusaidia juhudi za mchakato wa amani kuendelea.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,RTRE
Mhariri: Yusuf, Saumu