1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiga kura Ulaya wafika vituoni siku ya mwisho ya uchaguzi

9 Juni 2024

Wapiga kura kote Ulaya wanapiga kura katika siku ya mwisho na kubwa zaidi ya uchaguzi wa bunge la Umoja wa Ulaya. Vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vinatarajiwa kupata mafanikio.

https://p.dw.com/p/4gpiK
Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya
Uchaguzi huo utatoa muelekeo wa Umoja wa Ulaya kwa miaka mitano ijayoPicha: Kenzo TRIBOUILLARD/AFP

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa katika nchi 21, zikiwemo Ufaransa na Ujerumani, kwa ajili ya uchaguzi huo ambao utatoa muelekeo wa Umoja wa Ulaya kwa miaka mitano ijayo.

Uchaguzi huu unajiri wakati bara la Ulaya linakabiliwa na vita vya Urusi nchini Ukraine, mivutano ya kimataifa ya kibiashara na kiviwanda inayotokana na ushindani wa Marekani na China, athari za mabadiliko ya tabianchi na nchi za Magharibi ambazo katika miezi michache ijayo huenda itabidi zizoee utawala mpya wa Donald Trump.

Soma pia: Uchaguzi wa Bunge la Ulaya kudhoofisha muungano wa Scholz?

Zaidi ya raia milioni 360 wanastahili kupiga kura kote katika mataifa 27 wanachama wa Umoja wa UIaya. Uchaguzi huo ulianza Alhamisi wiki hii, ijapokuwa ni kundi dogo tu linalotarajiwa kupiga kura zao. Matokeo yatatoa sura ya muundo wa Bunge lijalo la Umoja wa Ulaya ambalo husaidia katika kuamua nani anayeongoza Halmashauri Kuu ya Ulaya, ambapo kiongozi wa kihafidhina wa Ujerumani Ursula von der Leyen anagombea kwa muhula wa pili. Matokeo ya awali yanatarajiwa kutolea leo jioni.