Wapiganaji wa M23 wanazidi kuuzingira mji muhimu wa Goma
22 Januari 2025Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) lilikiri Jumanne kuwa waasi wa M23 wamefanikiwa “kupenya” mashariki mwa nchi, ambako kundi hilo linalopigana na vikosi vya serikali limetwaa mji wa kibiashara unaofikisha mahitaji jijini Goma.
Kuanguka kwa Minova mikononi mwa wapiganaji wa M23 wanaoungwa mkono na jeshi la Rwanda kunazidisha mzingiro wa jiji kuu la kikanda, Goma, katika mzozo ambao umewalazimisha mamia ya maelfu ya watu kukimbia makazi yao.
“Adui amefanikiwa kuvunja ulinzi katika maeneo ya Bweremana (Kivu Kaskazini) na Minova (Kivu Kusini),” alisema msemaji wa jeshi, Jenerali Sylvain Ekenge, katika taarifa ya nadra kutoka kwa maafisa wa jeshi.
Chanzo kimoja cha kijeshi kililiambia shirika la habari la AFP mapema siku ya Jumanne kwamba mapigano bado yanaendelea, lakini tayari kilikiri kuwa “adui ameitwaa Minova.”
Minova, mji wenye takriban wakazi 65,000, upo jimboni Kivu Kusini kati ya Ziwa Kivu na milima ya Masisi. “Waasi wa M23 waliwasili saa 12 asubuhi. Wakazi wameanza kukimbia,” alisema kiongozi wa jadi wa Minova, Shosho Ntale, katika mazungumzo na AFP kwa njia ya simu. Chanzo kimoja hospitalini na vyanzo kadhaa vya kibinadamu vilithibitisha pia kwamba M23 wameutwaa Minova.
Tangu kujitokeza upya mwishoni mwa 2021, vuguvugu la M23 limeendelea kujitanua katika eneo la mashariki mwa DRC. Lakini kutekwa kwa Minova ni sehemu ya msururu wa mafanikio makubwa ya hivi karibuni kwa kundi hilo.
Mapema Januari, wapiganaji wa M23 walilitwaa eneo la Masisi, makao makuu ya utawala ya wilaya ya Masisi katika jimbo la Kivu Kaskazini. Masisi ina takriban wakazi 40,000 na iko umbali wa kilomita 80 kutoka Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini.
Soma pia: Huduma za usafiri Goma zatatizika kufuatia mapigano yanayoendelea
Mapigano sasa yanaendelea katika maeneo kadhaa karibu na Goma, ambapo mamia ya maelfu ya watu wameyakimbia makazi yao na kujikusanya pembezoni mwa jiji hilo. Mwaka 2012, M23 ilifanikiwa kulidhibiti jiji la Goma kwa muda mfupi.
Kwa sasa, mapigano yaliyo karibu zaidi yako umbali wa kilomita 20 kutoka Goma, katika vilima vya Sake, hali inayozua wasiwasi juu ya mustakabali wa jiji hilo. Waandishi wa habari wa AFP wameripoti milipuko mikubwa kusikika hadi Goma tangu Jumatatu.
Hata hivyo, katika taarifa yake Jumanne, jeshi la DR Congo limesema “jeshi la Rwanda na vibaraka wake wa M23 wamezuiliwa na kurudishwa nyuma” katika eneo hilo.
Njia nyingi zinazoelekea Goma zimekatwa na mapigano, na wakazi wanalazimika kuvuka Ziwa Kivu, mara nyingi wakibeba bidhaa kwenye boti zilizozidi uwezo wake. Ajali za boti ni za kawaida katika ziwa hilo, na mara nyingi hakuna orodha kamili ya abiria.
Tangu Jumatatu asubuhi, boti zimekuwa zikiwasafirisha watu wanaokimbia Minova ambao wanajaribu kutafuta hifadhi Goma, kwa mujibu wa vyanzo vya eneo hilo.
Soma pia: Zaidi ya watu 100,000 wakimbia makaazi yao Kivu ya Kaskazini
“Tunaendelea kupokea wakimbizi wanaowasili kwa wingi,” alisema Ishara Kaziwa, anayesimamia ulinzi katika kambi ya Lushagala pembezoni mwa Goma. “Tayari tumepokea kaya zaidi ya 100,” aliongeza.
Zaidi ya watu 230,000 wamekimbia ghasia mashariki mwa DRC tangu mwanzo wa mwaka huu, kulingana na Umoja wa Mataifa, ambao Ijumaa iliyopita uliitaja hali hiyo kuwa miongoni mwa dharura za kibinadamu “zinazotia wasiwasi zaidi” ulimwenguni.
“Waasi wanasema wanatuletea amani na kwamba hatuna cha kuogopa,” mkazi mmoja wa Minova, ambaye hakutaka kutaja jina lake, aliiambia AFP kwa njia ya simu.
Hospitali moja mjini Goma imepokea zaidi ya watu 200 waliojeruhiwa tangu mapigano yalipozidi makali mapema Januari.