Washirika wa Ukraine wakutana Ramstein kujadili msaada zaidi
21 Aprili 2023Stoltenberg ameyasema hayo katika mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa jumuiya hiyo unaofanyika katika kituo cha jeshi la anga la Marekani kilichoko Ramstein magharibi mwa Ujerumani.
Mkutano huo umeitishwa na Marekani, na unazishirikisha nchi zipatazo 50 washirika wa Ukraine katika juhudi zake za kukabiliana na uvamizi wa Urusi.
Soma zaidi: Ukraine yatarajia maamuzi mazito kutoka Ramstein
Katibu Mkuu wa jumuiya ya NATO Jens Stoltenberg amesema vita vya Ukraine vilivyoingia katika mwaka wa pili vimegeuka kuwa vya msuguano, aina ya vita ambavyo kila upande unausubiri mwingine udhoofike kabisa.
Amesema ili kuisaidia Ukraine kupata ushindi inawabidi washirika wake sio tu kuipatia silaha mpya, bali kuhakikisha kuwa zilizopo zinaendelea kufanya kazi.
Marekani itangaza mwelekeo mpya katika kuisaidia Ukraine
Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin ambaye ndiye mwenyeji wa mkutano huo, amesifu mchango wa kundi la nchi zinazoisaidia Ukraine ambao umefikia thamani ya dola bilioni 55, na kuongeza kuwa juhudi sasa zinaelekezwa katika maeneo matatu.
''Katika mkutano wa leo tutajikita katika masuala matatu; ulinzi wa anga, risasi na makombora pamoja na uwezeshaji'', amesema Austin na kuongeza kuwa ''Ukraine inahitaji kwa hali ya dharura msaada wetu ili iweze kuwalinda raia wake na miundombinu dhidi ya kitisho cha makombota ya Urusi.''
Uanachama wa Ukraine katika NATO
Kwenye mkesha wa mkutano huo, rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy aliiomba jumuiya ya NATO kuzishawishi nchi wanachama ambazo bado zinasitasita kuipatia Ukraine ndege za kisasa pamoja na magari ya kivita, na akiihimiza pia jumuiya hiyo kuharakisha uanachama wa Ukraine.
Soma zaidi: Austin: Ukraine inaweza kuishinda Urusi
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amesema huu sio wakati muafaka wa kujadili uanachama wa Ukraine katika jumuiya ya NATO, hata kama mlango umefunguka kidogo. Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg ameunga mkono mtazamo huo, akisema kipaumbele ni kuhakikisha Ukraine inanusurika kwanza na kuendelea kuwepo kama nchi.
Siku moja kabla ya mkutano huu wa Ramstein, Stoltenberg alifanya ziara mjini Kiev, na Urusi imeishutumu ziara hiyo ikisema ni ushahidi tosha kuwa jumuiya ya NATO ilikuwa na dhamira ya kuimeza Ukraine.
Vyanzo: DPAE, AFPE