1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto 330,000 wamenyanyaswa kingono katika Kanisa Katoliki

5 Oktoba 2021

Ripoti ya uchunguzi juu ya unyanyasaji wa kingono nchini Ufaransa imefichua kuwa watoto wapatao 330,000 wamekuwa wakinyanyaswa kingono katika kanisa katoliki la Ufaransa kwa zaidi ya miaka 70 iliyopita.

https://p.dw.com/p/41H0x
Kardinal Philippe Barbarin, Erzbischof von Lyon
Padri Philippe Barbarin akiongoza ibada ya misa katika kanisa mjini Lyon, UfaransaPicha: Robert Deyrail/abaca/picture alliance

Mkuu wa tume iliyotoa ripoti hiyo Jean-Marc Sauve amesema idadi hiyo ya watoto walionyanyaswa kingono, kulingana na utafiti wa kisayansi, inahusisha unyanyasaji uliofanywa na mapadri, makasisi pamoja na wafanyikazi wa kawaida katika kanisa hilo. 

Ufichuzi huo ni wa hivi karibuni kulitikisa Kanisa Katoliki baada ya kuzongwa na kashfa za unyanyasaji wa kingono kote duniani, mara nyingi zikihusisha watoto, kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Jean-Marc Sauve, mkuu wa tume iliyotoa ripoti hiyo, aliiwasilisha hadharani ripoti yenyewe na kusema unyanyasaji huo ulikuwa ni wa kimfumo.

Soma pia: Papa Francis ahimiza amani kwa wote Iraq

Mbele ya vyombo vya habari vya Ufaransa, Sauve amesema theluthi mbili ya mapadri ambao ni takriban 3,000 wamekuwa wakifanya kazi katika Kanisa Katoliki kwa zaidi ya miaka 70 iliyopita wanatuhumiwa kuhusika katika kashfa hiyo.

Jean-Marc Sauve amesema, "Juu ya yote, Kanisa lilipuuza, lilikaa kimya, lilikuwa linaziba ukweli juu ya suala hili. Tume ilijadili kwa muda mrefu na imefikia hitimisho la pamoja: Kanisa halikujua jinsi ya kuona, jinsi ya kusikia, wala halikujua jinsi ya kufuatilia ishara za wazi."

Sauve ameongeza kuwa, kando la Kanisa kutochukua hatua stahiki za kuzuia unyanyasaji huo lakini pia lilifumbia macho visa hivyo vya unyanyasaji kwa kushindwa kuripoti bali hata wakati mwengine kuwapeleka watoto hao kwa watu waliokuwa wakiwadhulumu kingono.

Tatizo hilo la unyanyasaji wa kingono bado lingalipo.

Frankreich | PK Untersuchungskommission zum Kindesmissbrauch in der katholischen Kirche in Frankreich
Mkuu wa tume iliyotoa ripoti ya ufichuzi wa kashfa ya ngono, Jean-Marc SauvePicha: Thomas Coex/AFP/Getty Images

Sauve amesema tume hiyo imepata takriban waathiriwa 2,700 wa visa vya unyanyasaji lakini kulingana na tafiti mbalimbali na pia kwa kuuliza makundi mengine ya watu, huenda idadi ya waathiriwa ikawa karibu 216,000. Idadi hiyo huenda ikaongezeka hadi 330,000 ukijumuisha udhalilishaji uliofanywa na wafanyikazi wa kawaida kwenye Kanisa Katoliki.

Tume hiyo ilianzishwa na maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Ufaransa mwishoni mwa mwaka 2018 ikitwikwa jukumu la kutoa mwanga juu ya dhulma na unyanyasaji wa kingono na pia kurejesha imani ya umma kwa Kanisa, katika wakati ambapo idadi kubwa ya waumini walikuwa wanakwepa kuhudhuria ibada.

Soma pia: Kanisa Katoliki latangaza sheria mpya kuhusu unyanyasaji wa kingono

Padri Andri azungumzia unyanyasaji wa kingono kanisani

Sauve hata hivyo amesema tatizo hilo bado lingalipo. Mkuu huyo wa tume iliyochunguza dhulma hizo, ameongeza kuwa hadi miaka ya 2000, Kanisa Katoliki halikuonyesha kujali waathiriwa wa unyanyasaji huo na kwamba lilianza kubadili mtazamo wake mnamo mwaka 2015-2016.

Amesema baadhi ya kesi hizo za dhulma zimewasilishwa kwa waendesha mashtaka japo nyengine zaidi ya 40 ni za zamani sana japo zinahusisha watuhumiwa ambao bado wako hai, na kwamba tayari zimewasilishwa kwa maafisa wa kanisa katoliki.

Maaskofu wakuu wa Ufaransa, katika ujumbe wao kwa waumini wakati wa misa ya Jumapili, walisema ripoti hiyo ni kipimo cha ukweli na kuwa ni wakati mgumu na mzito.