1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 21 wafariki kufuatia mvua kubwa Jamhuri ya Dominica

20 Novemba 2023

Takriban watu 21, wakiwemo watoto watatu, wamefariki kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika Jamhuri ya Dominica mwishoni mwa juma.

https://p.dw.com/p/4Z9oQ
Kimbunga Fiona kimesababisha mvua kubwa katika Jamhuri ya Dominika na Puerto Rico
Watu wakijikinga dhidi ya mvua mjini Higuey, Jamhuri ya DominikaPicha: Ricardo Rojas/REUTERS

Dhoruba kubwa iliyotokea katika muda wa saa 48 zilizopita imesababisha mafuriko, imeharibu miundombinu na kuangusha nyumba kadhaa katika taifa hilo la Caribbean, katika kile Rais Luis Abinader alichokiita kama "tukio kubwa zaidi la mvua kuwahi kunyesha" katika historia ya nchi hiyo.

Ubalozi wa Marekani umetoa tahadhari na kueleza kwamba, mvua hizo zinatarajiwa kuendelea kunyesha katika maeneo mengine ya taifa hilo kwa saa 24 zijazo.

Katika tukio lililotokea jana, ukuta uliangukia magari kadhaa kwenye barabara katika mji mkuu wa Santo Domingo, na kuua watu tisa. Watu wengine tisa walipoteza maisha katika matukio tofauti huko Santo Domingo.

Kulingana na kituo cha oparesheni za dharura, takriban watu 13,000 wamehamishwa huku mikoa mengi kati ya 32 ya taifa hilo yakiwekwa chini ya tahadhari.