Watu waondolewa kwa lazima katika maeneo ya migodi Kongo
12 Septemba 2023Katika ripoti yenye kurasa 98, shirika la Amnesty na lile la Kongo IBGDH ( Initiative pour la Bonne Gouvernance et les Droits Humains) yamegundua kuwa jamii zinazoishi karibu na miji yenye migodi kama Kolwezi, jimboni Lualaba,kusini Mashariki mwa Kongo, hulazimishwa kuyahama makazi yao ili kupisha miradi ya uchimbaji madini.
Jamii zalazimishwa kuhama
Jean-Mobert Senga, mtafiti wa shirika la Amnesty International nchini Kongo na mmoja wa waandaaji wa ripoti hiyo amesema mamia ya raia wamehamishwa kwenye makaazi yao pasina hiyari yao.
''Ni vigumu sana kujua kwa usahihi ni watu wangapi waliondolewa kwenye makazi."
Alisema Senga na kuongeza kuwa wanachofahamu kwa sasa ni mamia ya wakaazi walihamishwa na maeneo yao kuondolewa kwenye ramani.
Alisema katika utafiti wao waligundua miradi minne mikubwa ambayo inaendeshwa na makampuni ya kimataifa, kuhusika katika kadhia hiyo.
''Lakini, mbali na kampuni hizi, ukiukaji huu pia unafanywa na mamlaka za Kongo."
Alisisitiza kuwa kampuni hizo za ndani zinazo wajibu kisheria na kisera kulinda haki za raia wake.
Ripoti hiyo ya Amnesty International ambayo ilifanyika kwa kipindi cha miaka miwili, na kuwahoji watu takriban 130.
Miongoni mwa waliohojiwa ni pamoja na waathiriwa wa shughuli za uchimbaji madini huko Kolwezi.
Ripoti hiyo ambayo imezua mjadala ndani na nje ya Kongo, imesisitiza kuwa waathirika wote wanapaswa kunufaika na uchimbaji wa madini hayo.
Vitendo vya dhuluma vikomeshwe
Watafiti wa mashirika ya na IBGDH waligundua ukiukaji wa mara kwa mara wa ulinzi wa kisheria na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu, pamoja na kupuuzwa wazi kwa mwongozo wa Umoja wa Mataifa kuhusu kanuni za biashara na haki za binadamu.
Katibu Mkuu wa Amnesty International Agnes Callamard amesema shirika hilo linatambua hitaji muhimu la kuelekea kwenye matumizi ya nishati mbadala lakini linalenga kukomesha vitendo vya dhuluma dhidi ya raia wa Kongo.
Sheria na Kanuni za madini nchini Kongo ambazo zilifanyiwa marekebisho mwaka wa 2018, zinatoa fursa ya kufukuzwa au kuhamishwa kwa watu kutokana na uchimbaji madini.
Lakini sheria hizo, kama kanuni zingine za kimataifa, zinatoa mbinu za kulinda haki za watu au jamii husika.
Ripoti ya shirika la Amnesty imesema mbali na kwamba harakati yenyewe sio haramu, lakini hali ambayo inafanywa huko Kongo inakiuka sheria za kitaifa na za kimataifa. Katika visa vitatu kati ya vinne vilivyochunguzwa, shirika la Amnesty limesema baadhi ya jamii hufukuzwa bila mashauriano, wakati mwingine bila hata kufahamishwa, na bila njia yoyote ya kukata rufaa, au kwa vyovyote vile bila kulipwa fidia.