Watu wanane wauawa na vikosi vya usalama nchini Sudan
1 Julai 2022Tume ya Madaktari wa Sudan imesema katika taarifa yake waliyoitoa kupitia ukurasa wa Twitter kwamba raia sita waliuawa kwa kupigwa risasi wakati polisi walipofyatua risasi za moto dhidi ya waandamanaji huko Omdurman ambao ni mji pacha wa mji mkuu wa Khartoum. Mwandamanaji mwingine alifariki mjini Khartom kutokana na majeraha ya risasi ya kichwa na mtoto mmoja pia amepoteza maisha kutokana na risasi ya kifua.Sudan: Waandamanaji wawili wauawa kwa kupigwa risasi
Mjini Khartoum, polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi kutawanya maelfu ya waandamanaji ambao walikuwa wanajaribu kufika ikulu ya rais. Vidio zilizosambaa mitandaoni zimewaonyesha waandamanaji wakipeperusha bendera ya Sudan na kukimbia chini ya wingu zito la mabomu ya machozi. Video nyingine zilionyesha waandamanaji waliobeba mabango yanayosomeka "hakuna majadiliano! hakuna ushirikiano! wakirejelea upinzani wa kugawana madaraka na watawala wa kijeshi.
Abdel Azeem Hassan ni mchambuzi wa kisiasa na kisheria wa Sudan anasisitiza kuwa suluhisho pekee ni viongozi wa kijeshi kuruhusu utawala wa kiraia "Mamilioni ya watu waliomiminika mitaani tangu mwaka 2019, wamekuwa na lengo moja, nalo ni kupata serikali kamili ya kiraia, ambapo mamlaka yapo mikononi mwa watu, na kwamba wanajeshi warejee kwenye kambi zao. Umati huu umekusanyika kusema jambo moja kwamba wanataka serikali kamili ya kiraia. Watu hawa wamezungumza na wanasema wataendelea na njia hii hadi malengo ya mapinduzi ya desemba yatakapotimia."
Makundi ya Sudan yanayoongoza katika kudai demokrasia yaliitisha maandamano ya nchi nzima siku ya Alhamis kusisitiza madai yao ya kubatilisha mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 25. Maandamano hayo pia yameangukia katika kumbukumbu ya miaka mitatu ya maandamano ya umma ya mwaka 2019 yaliyomwondoa mamlakani kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir na kuwalazimu viongozi wa kijeshi kuketi meza moja na makundi ya wanaodai demokrasia na hatimaye kusaini makubaliano ya kushirikiana madaraka. Makubaliano hayo yalitarajiwa kuiongoza Sudan wakati wa kipindi cha mpito, hadi uchaguzi mkuu utakapofanyika. Lakini mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Oktoba yalivuruga utaratibu huo.Sudan: Vikosi vya usalama vyatumia gesi ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji
Mtandao wa intaneti na mawasiliano ya simu vilitatizika tangu majira ya asubuhi hapo jana, hatua ambayo mamlaka ya Sudan mara nyingi huitumia ili kuzuia mikusanyiko ya watu wengi. Umoja wa Afrika, Jumuiya ya kikanda IGAD, Umoja wa Mataifa zimekuwa zikijaribu kuwezesha mazungumzo kati ya viongozi wa kijeshi na raia, lakini mazungumzo hayo yamesusiwa na makundi makuu ya kiraia.