Yvonne Aki-Sawyerr, mshindi wa tuzo ya Ujerumani kwa Afrika
17 Oktoba 2024Tangu Aki-Sawyerr alipoingia madarakani na kuwa Meya wa Freetown, miaka sita iliyopita, jiji hilo ambalo liliharibiwa kwa miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, tayari limebadilishwa kuwa mahali pazuri pa kuishi; nyumba, usambazaji wa maji na ukusanyaji wa taka umeimarishwa kwa kiasi kikubwa.
Yvonne Aki-Sawyerr ameiambia DW kwamba alikulia kwenye mji wa kijani, na alipenda kupanda miti hata alipokuwa mdogo. Kumbukumbu hizo za mji mkuu wa Sierra Leone, Freetown, na maono ya kulirejesha jiji katika hadhi yake ya zamani, zilikuwa sababu kuu za Aki-Saywerr kuamua kugombea umeya.
"Unapoona kwamba yote yanaharibiwa, pamoja na matatizo ya maji taka kwa wakati huo, hicho ndicho kilikuwa chanzo kilichonisukuma mimi kugombea," amesema Aki-Sawyerr.
Dhamira ya maendeleo endelevu ya miji
Kulingana na Wakfu wa German Afrika, DAS, mwanamazingira huyo mwenye umri wa miaka 56, anatekeleza maono yake ya mtaji unaoweza kuishi, wa haki na ulio endelevu. Aidha, ametambua dhamira yake isiyoyumba ya maendeleo endelevu ya miji na ushiriki wa ndani wa Tuzo ya Ujerumani kwa Afrika, mwaka 2024.
Unaweza kusoma pia: Vuguvugu la wanawake la Cameroon lashinda Tuzo ya Ujerumani kwa Afrika
Spika wa Bunge la Ujerumani, Bärbel Bas aliikabidhi tuzo hiyo kwa Aki-Sawyerr jana usiku. Mwanamazingira huyo aliwashinda wagombea wengine kadhaa katika jopo huru lililokuwa na majaji 20.
Tangu mwaka 1993, Wakfu wa German Africa, umekuwa ukiwatunuku watu mbalimbali kutokana na juhudi zao kuelekea katika demokrasia, amani, masuala ya kijamii, haki za binaadamu, maendeleo endelevu, utafiti, sanaa na utamaduni barani Afrika. Taasisi isiyoegemea upande wowote inasema kuwa meya huyo amejitolea zaidi kuliko ofisi yake inavyohitaji.
Yvonne Aki-Sawyerr anaelewa kile anachokitaka, na akachukua hatua kulingana na Imani yake ya ndani. Jiji la kijani la enzi za utoto wake linapaswa kubaki hivyo kwa vizazi vijavyo.
Wasifu wa Aki-Sawyerr
Baada ya kusoma Sierra Leone na Uingereza, alianza kazi yenye matumaini katika sekta ya fedha, akifanya kazi kama mtaalamu wa fedha na mkaguzi wa hesabu huko London, kwa zaidi ya miaka 25. Hata hivyo, wakati nchi yake ilipokumbwa na mripuko wa ugonjwa wa Ebola mwaka 2014, alirejea Freetown, jiji la bandari lenye wakaazi zaidi ya milioni moja, akifanya kazi kama meneja anayeshughulikia mizozo.
Unaweza pia kusoma: Wanasayansi wawili wa Afrika watunukiwa Tuzo ya Ujerumani
Wakati huo aliwashinda wagombea watano wa kiume, na mpango wake wa miaka minne wa "Ibadilishe Freetown", na akawa mwanamke wa kwanza kuliongoza jiji hilo. Aki-Saywerr aliilekeza ofisi yake kurekebisha matatizo makubwa ya taka na kupanda miti Freetown. Aki-Sawyerr anasema jiji hilo sasa linagawa hadi miti 25,000.
Chochote ambacho meya huyo anakishughulikia, wakaazi wanahusishwa. Mtindo huu wa usimamizi unaowahusisha raia umemletea Aki-Sawyerr kutambulika ndani na kimataifa. Aki-Sawyerr ameiambia DW kuwa bado wana jukumu kubwa la kufanya.
"Freetown ni jiji la miti. Lengo letu lilikuwa kupanda miti milioni moja," amesema Aki-Sawyerr.
Mpango wa kupanda miti milioni moja
Mwanzoni mwa 2020, Aki-Sawyerr alizindua kampeni ya "Freetown Jiji la Miti" kwa lengo kuu la kupanda miti milioni moja Freetown ndani ya miaka miwili. Amekaribia kufikia lengo hilo, kwani amefanikiwa kupanda miti 997,000. Miti mingi mipya inapunguza viwango vya joto na kuongeza uwezo wake wa kustahimili mafuriko.
Aki-Sawyerr anasisitiza kuwa lengo lake sio tu kukabiliana na matatizo ya kimazingira, lakini anaamini ni muhimu kutambua jinsi matatizo ya mazingira yanavyoyafanya maisha ya wakazi wa Freetown kuwa magumu zaidi.
Unaweza pia kusoma: Rais wa zamani wa Sierra Leone ashtakiwa kwa uhaini
Mwaka 2023, hakuchaguliwa tu kuwa meya kwa muhula wa pili, lakini pia alikuwa mwenyekiti mwenza wa Miji C40, vuguvugu ambalo kwa sasa analiongoza na Meya wa London, Sadiq Khan. C40, ni mtandao wa kimataifa wa takribani mameya 100 wa miji mikuu duniani, inayofanya kazi pamoja ili kukabiliana na mzozo wa hali ya hewa.
Waandishi: Silja Fröhlich / Blaise Eyong