Zaidi ya watu 120 wauawa katika ghasia za RSF-Sudan
27 Oktoba 2024Umoja wa Mataifa na kundi la Madaktari nchini Sudan wamesema zaidi ya watu 120 waliuawa katika mji mmoja, wakati wa shambulizi lililofanywa na wanamgambo wa RSF siku chache zilizopita. Hilo ni shambulizi la hivi karibuni kufanywa na RSF dhidi ya wanajeshi wa Sudan baada ya kukumbwa na msururu wa mashambulizi na kupoteza udhibiti katika eneo hilo.
Soma: UN: Nusu ya raia wa Sudan wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula
Umoja wa Mataifa ulisema katika taarifa yake kuwa wapiganaji wa RSF walivamia vijiji na miji upande wa mashariki na kaskazini mwa jimbo la Gezira kati ya Oktoba 20-25. Wanadaiwa kuwafyatulia risasi raia na kuwanyanyasa kingono wanawake na wasichana, na kupora mali za umma na binafsi. Mratibu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wa Sudan Clementine Nkweta-Salami, amesema mashambulizi hayo yanafanana na yale yaliyotokea mkoani Darfur mwanzoni mwa miaka ya 2000.