Zaidi ya watu 120 wauawa katika mji wa Sariha nchini Sudan
28 Oktoba 2024Katika taarifa, muungano huo wa madaktari umesema kuwa takriban watu 124 waliuawa na wengine 200 walijeruhiwa katika mji huo wa Sariha na kuongeza kuwa wanamgambo hao wa RSF pia waliwakamata watu wengine 150.
Picha zilizosambaa mtandaoni, zingine zikisambazwa na kundi hilo la RSF lenyewe, zilionesha wafuasi wa kundi hilo wakiwadhulumu watu waliowazuia. Video moja ilionyesha mwanaume aliyevalia sare za kijeshi akimshika mzee mmoja kidevu na kumburuta huku watu wengine wenye silaha wakiimba.
Hata hivyo, RSF haikujibu mara moja madai hayo, baada ya kutolewa ombi la kufanywa hivyo.
Muungano wa madaktari waitaka UN kuishinikiza RSF kufungua barabara salama
Muungano huo wa madaktari, umetoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulishinikiza kundi la RSF kufungua barabara salama ili kuwezesha makundi ya msaada kuwafikia watu katika vijiji vilivyoathirika.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa hakuna njia ya kuwasaidia waliojeruhiwa ama kuwahamisha kwa matibabu.
Kabla ya zaiara yake nchini Sudani wiki ijayo, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM, Amy Pope, ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba mauaji hayo na ukiukaji wa kutisha wa haki za binadamu huko Gezira, vinazidisha mateso yasiokubalika dhidi ya binadamu kwa raia wa Sudan.
Pope ametoa wito wa juhudi za pamoja za kimataifa za kumaliza mzozo huo huku akiongeza kuwa hakuna muda wa kupoteza na maisha ya mamilioni ya watu yamo hatarini.
Katika taarifa siku ya Jumamosi, mratibu wa masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifanchini Sudan Clementine Nkweta-Salami, aliyataja mashambulizi hayo kuwa makosa ya jinai na kuongeza kuwa wanawake, watoto na wasiojiweza wanaathirika zaidi kutokana na mzozo huo ambao tayari umesababisha idadi kubwa ya vifo.
Mashambulizi ya RSF yanafanana na mauaji ya halaiki ya Darfur mwanzoni mwa miaka ya 2000
Nkweta-Salami amesema mashambulizi hayo yanafanana na yale ya kutisha yaliyofanywa wakati wa mauaji ya halaiki ya Darfur mwanzoni mwa miaka ya 2000, ikiwa ni pamoja na ubakaji, unyanyasaji wa kingono, na mauaji ya watu wengi.
Katika taarifa siku ya Jumamosi, Umoja wa Mataifa ulisema kuwa wapiganaji hao waRSF walivamia vijiji na miji upande wa mashariki na kaskazini mwa jimbo la Gezira kati ya Oktoba 20 na 25, huku wakiwafyatulia risasi raia na kuwanyanyasa kingono wanawake na wasichana. Umoja huo umeongeza kuwa wanamgambo hao pia walipora mali za umma na kibinafsi zinazojumuisha masoko ya wazi.
Mapigano mapya yautikisa mji mkuu wa Khartoum
Kulingana na takwimu za ufuatiliaji wa wahamiaji za IOM, zilizotolewa jana Jumapili, mashambulizi yamesababisha watu 46,500 kupoteza makazi yao katika mji wa Tamboul na vijiji vingine mashariki na kaskazini mwa Gezira wiki iliyopita.