1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 80 wauwa katika shambulizi Ethiopia

14 Januari 2021

Tume ya kitaifa ya haki za binadamu nchini Ethiopia imesema zaidi ya raia 80 wameuwawa katika shambulizi lililofanyika magharibi mwa Ethiopia. Eneo hilo limeshuhudia mauaji ya mara kwa mara katika miezi ya hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/3nunu
Sudan Konflikt Tigray | Abrahaley Minasbo, Überlebender
Picha: Nariman El-Mofty/AP Photo/picture alliance

Mauaji hayo yatamuongezea shinikizo Waziri Mkuu Abiy Ahmed atumie nguvu zaidi kuingilia kati machafuko hayo ya eneo la Benishangul-Gumuz, linalopakana na Sudan na Sudan Kusini. eneo hilo pia ndiko uliko mradi mkubwa wa kufua umeme wa nchi hiyo katika mto wa Blue Nile.

Mshauri na msemaji wa tume ya kutetea haki za binadamu ya Ethiopia Aaron Maasho amesema shambulizi hilo lilifanyika kati ya saa kumi na moja alfajiri na saa moja asubuhi huku wahanga wakiwa kati ya umri wa miaka miwili na arubaini na tano. Amesema tume hiyo ambayo ni huru ila ina uhusiano na serikali, bado inachunguzi waliofanya mauaji hayo na jinsi watu hao walivyouwawa.

Machafuko yamechochewa kikabila

Mtu mmoja aliyeponea shambulizi hilo, Ahmed Yimam, ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa, alihesabu miili 82 na wengine 22 waliojeruhiwa. Amesema silaha kubwa iliyotumika kulifanya shambulizi hilo ilikuwa ni visu ingawa nyuta na bunduki pia zilitumika. Yimam amedai kwamba anahofia mashambulizi zaidi kwa kuwa wanaotekeleza mauaji hayo hawaadhibiwi na hakuna serikali za mitaa zinazofanya kazi kwa sasa.

Äthiopien Abiy Ahmed
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: Amanuel Sileshi/AFP

Viongozi wa upinzani nchini Ethiopia wameyaelezea machafuko ya huko Metekel kama yaliyochochewa kikabila, wakidai wanamgambo wa kabila la Gumuz wanafanya kampeni ya kuwashambulia watu wa makabila mengine likiwemo kabila la Amhara ambalo ni la pili kwa ukubwa nchini humo.

Dessalegn Chanie, ambaye ni mwanachama mkuu katika chama cha upinzani cha Nationa Movement for Amhara, ameliambia shirika la habari la AFP Alhamis kuwa anashuku viongozi katika eneo hilo wanashirikiana na wavamizi ingawa hakutoa ushahidi wowote kuhusiana na madai hayo.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed ameshindwa kuleta amani

Raia wa Metekel wameshuhudia mauaji katika eneo hilo tangu Septemba mwaka jana huku shambulizi la Desemba 23 likishuhudia watu 207 kuuwawa.

Kufikia sasa Waziri Mkuu Abiy ameshindwa kuleta amani katika eneo hilo au hata kuelezea kile kinachosababisha machafuko hayo. Haya ni licha ya kulitembelea eneo hilo mwezi Desemba na kuamrisha jeshi kudumisha usalama eneo hilo.

Sudan Konflikt Tigray | Hiwet Aregawi, Überlebender
Kijana wa Kiethiopia aliyeshambuliwa na wanamgamboPicha: Nariman El-Mofty/AP Photo/picture alliance

Hakuna uhusiano kati ya mashambulizi hayo na mapigano yanayoendelea kaskazini mwa Ethiopia katika eneo la Tigray ambapo Abiy alituma vikosi vya majeshi mwezi Novemba kuwakamata na kuwapokonya silaha viongozi wa chama tawala eneo hilo kinachoipinga serikali ya Ethiopia.