1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky asifu ujasiri wa Ukraine siku 500 za vita

Sylvia Mwehozi
9 Julai 2023

Rais Volodymyr Zelensky ameipongeza nchi yake ya Ukraine aliyoitaja kuwa jasiri katika siku ya 500 ya uvamizi wa Urusi jana Jumamosi wakati kukiripotiwa vifo vya watu wanane kufuatia shambulio la kombora la Urusi.

https://p.dw.com/p/4TdR1
Ukraine, Lviv| Zelensky
Rais Volodymyr Zelensky katika tukio la kurejea kwa makamanda wa UkrainePicha: Ukrainian Presidential Press Service/Handout/AFP

Rais Volodymyr Zelensky ameipongeza nchi yake ya Ukraine aliyoitaja kuwa jasiri katika siku ya 500 ya uvamizi wa Urusi jana Jumamosi, wakati kukiripotiwa vifo vya watu wanane kufuatia shambulio la kombora la Urusi. Rais Zelensky jana jumamosi alikamilisha ziara yake nchini Uturuki ambapo alipata uungwaji mkono wenye matumaini juu ya azma ya nchi yake kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Aidha, kiongozi huyo pia amepata ahadi ya Marekani ya kupelekewa mabomu ambayo yanaweza kuleta uharibifu mkubwa kwa vikosi vya Urusi kwenye uwanja wa vita. Wakati akirejea kutoka Uturuki, Zelensky pia aliwarudisha makamanda watano wa Ukraine ambao walipaswa kubaki Uturuki hadi mwisho wa mzozo chini ya makubaliano ya kubadilishana wafungwa. Urusi tayari imelaani juu ya kuachiliwa kwa makamanda hao.