1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky ataka Ukraine isaidiwe kama inavyosaidiwa Israel

16 Aprili 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, amewahimiza washirika wake kuonyesha kile alichokiita “mshikamano au umoja” kwa Ukraine kama Israel, ambao ulizuia shambulio la Iran mwishoni mwa juma kwa msaada wa nchi za Magharibi.

https://p.dw.com/p/4eqUH
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky Picha: Gints Ivuskans/AFP

Kupitia taarifa aliyochapisha kwenye ukurasa wake wa Telegram, Zelensky aliwashukuru washirika walioitikia wito wa Ukraine wa ulinzi zaidi wa anga lakini akasema: "Nguvu ya mashambulizi ya Urusi inahitaji umoja zaidi".

Zelensky ameongeza kuwa kwa kuilinda Israel, ulimwengu huru umedhihirisha kwamba umoja huo hauwezekani tu, bali pia kwa ufanisi kwa asilimia mia moja, vivyo hivyo inawezekana katika kuilinda Ukraine, ambayo, kama Israeli, sio mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Soma pia:Halmashauri ya UIaya yaidhinisha mipango ya meguzi ya Kiev

Katika tukio tofauti Halmashauri Kuu ya UIaya imeidhinisha mipango ya mageuzi ya Ukraine inayohitajika ili kutoa fedha zaidi kutoka kwa mpango wake wa msaada wa mabilioni ya euro. 

Halmashauri hiyo imetoa tathmini chanya ya mageuzi mapana ya Ukraine na mkakati wa uwekezaji kwa miaka minne ijayo, hatua inayofungua njia kwa nchi hiyo iliyo chini ya uvamizi wa Urusi, kupewa msaada wa mara kwa mara.