1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky avitaka vikosi vya Urusi viondoke Kherson

30 Agosti 2022

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ameyataka majeshi ya Urusi kukimbia kutoka kwenye eneo la kusini ili kuyaokoa maisha yao, baada ya vikosi vyake kuanzisha mashambulizi ya kulikomboa eneo hilo.

https://p.dw.com/p/4GEWt
Ukraine Kiew | Pressekonferenz: Wolodymyr Selenskyj
Picha: Ruslan Kaniuka/Ukrinform/ABACA/picture alliance

Majeshi ya Ukraine Jumanne yameendeleza operesheni iliyoanza Jumatatu kwa lengo la kulikomboa tena eneo la kusini linalodhibitiwa na Urusi na Zelensky amesema majeshi yake yanalinyakua tena eneo lao na hivyo kuwataka wanajeshi wa Urusi kwenda nyumbani.

''Nina uhakika wote mnaelewa kinachoendelea na kile tunachokipigania na tunachokitaka. Wanajeshi wetu hawahitaji kujitangaza. Ukraine inayarejesha maeneo yake ya Kharkiv, Lugansk, Donetsk, Zaporizhzhia na Kherson, Crimea na kwa hakika maeneo yetu katika Bahari Nyeusi na Bahari ya Azov,'' alifafanua Zelensky.

Hata hivyo, msemaji wa ikulu ya Urusi, Kremlin, Dmitry Peskov amesema Jumanne kuwa Urusi imefanikiwa kuzuia operesheni hiyo na kuwasababisha hasara kubwa wanajeshi wa Ukraine. Amesema Urusi ilikuwa ikizidi kusonga mbele na mipango yake nchini Ukraine na kwamba malengo yao yote yatafikiwa.

Katika wiki za kwanza za vita, Urusi iliyadhibiti maeneo ya kusini mwa Ukraine, karibu na pwani ya Bahari Nyeusi, ikiwemo mji wa Kherson ulioko kaskazini mwa Rasi ya Crimea ambayo Urusi ilijinyakulia.

Kremlin imeonya kuchukua hatua iwapo EU itazuia kutoa visa kwa raia wa Urusi 

Georgien Russland stoppt Ausgabe von Visa für georgische Staatsbürger
Picha: picture-alliance/ dpa

Ama kwa upande mwingine, ikulu ya Urusi, Kremlin imeonya kuwa itachukua hatua iwapo Umoja wa Ulaya utazuia kutoa visa kwa raia wa Urusi wanaosafiri kwenda katika nchi za umoja huo, kama sehemu ya kuiunga mkono Ukraine. Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov amesema wanajua kuna maoni tofauti miongoni mwa wananchi wa Ulaya kuhusu suala hilo na wanalifuatilia kwa karibu.

Wazo la kupiga marufuku watalii wa Urusi kuingia Ulaya limezigawa nchi za Umoja wa Ulaya, huku baadhi yao wakikubaliana nalo na wengine wakipinga, wakihofia kuwa litafunga milango kwa wapinzani wa Urusi wanaotaka kuikimbia nchi yao.

Soma pia: Mashambulizi yatokea tena karibu na kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia

Mawaziri wa mambo ya nje wa umoja huo watalijadili suala hilo katika mkutano wa siku mbili unaoanza Jumanne mjini Prague.

Aidha, Halmshauri Kuu ya Umoja wa Ulaya imesema leo kuwa umoja huo umetoa zaidi ya vidonge milioni tano vya potassium iodide kwa Ukraine ili kuilinda dhidi ya hatari ya mionzi. Kamishna wa umoja huo anayesimamia migogoro, Janes Lenarcic amesema kutokana na mashambulizi ya makombora yanayoendelea karibu na kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia, vidonge hivyo ni uwasilishaji wa awali ili kuwalinda raia.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umesema meli iliyopakia ngano kutoka Ukraine kuelekea katika eneo la Pembe ya Afrika ambalo limekumbwa na ukame, imetia nanga Jumanne, ikiwa ni meli ya kwanza kuwasili tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine miezi sita iliyopita. Meli hiyo imepakia tani 23,000 za nafaka na itafatiwa na meli nyingine yenye tani 7,000.

Meli ya UN iliyobeba nafaka yaelekea Afrika kutoka Ukraine

Jumla ya shehena katika meli hiyo ambayo itapakuliwa Djibouti na kusafirishwa hadi Ethiopia, inatosha kuwalisha watu milioni 1.5 kwa mwezi mmoja.

Huku hayo yakijiri, Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amesema hatua za serikali kuhakikisha usambazaji wa gesi wakati wa majira ya joto zimeitayarisha Ujerumani kukabiliana na vizuizi zaidi vya usambazaji wa gesi kutoka Urusi.

Matamshi hayo ameyatoa Jumanne, siku moja kabla Urusi haijasitisha usambazaji wa gesi kwa siku tatu.