Marekani yaidhinisha msaada kwa Ukraine
24 Aprili 2024Rais Joe Biden ndiye anayetakiwa kukamilisha mchakato huo kwa kutia saini na ameapa kuwa vifaa zaidi vitawasilishwa haraka kwenye eneo la vita huko Ukraine.
Tayari Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameipongeza hatua hiyo ya Baraza la Seneti kuidhinisha karibu dola bilioni 61 kwa taifa hilo ili kuisaidia kukabiliana na uvamizi wa Urusi. Kumeidhinishwa pia fedha za msaada wa kibinaadamu unaohitajika kwa Gaza, Sudan na Haiti.
Katika jumla ya msaada huo wa dola bilioni 95, kiasi dola bilioni 61 zimetengwa kwa ajili ya jeshi la Ukraine ambalo linahitaji mno silaha na wanajeshi wapya.
Soma pia: Ukraine yasifu Bunge la Marekani kuidhinisha msaada wa kijeshi
Muswada huo unaotarajiwa kuwa sheria umeafiki kutoa pia dola bilioni 26 za msaada kutokana na vita vya Israel na dola bilioni 8 ili kukabiliana na ushawishi unaoongezeka wa China huko Taiwan na katika kanda ya Indo-Pacific.
Muswada huo umejumuisha pia uwezekano wa kuupiga marufuku mtandao wa kijamii wa TikTok nchini Marekani, ikiwa wamiliki wa China hawatouza hisa zao ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
(Vyanzo: DPAE, AFPE)