Borrell: Vita vya Gaza ni "janga"
10 Septemba 2024Mkuu huyo wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya ametoa wito wa kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa nchi za kiarabu katika kushughulikia mzozo huo na kusisitiza kuwa mzozo huo hauna mstakabali ulio mwema:
"Umoja wa Ulaya umeunga mkono kikamilifu juhudi zinazoendelea za Misri, Qatar na Marekani. Lakini makubaliano ya kusitisha mapigano kwa kuzingatia mpango wa rais Biden bado hayajasainiwa na hakuna dalili kuwa yatasainiwa hivi karibuni. Na hii ni kwa sababu wale wanaopigana hawana nia ya kuvimaliza vita hivi na wamekuwa kila mara wakitafuta vijisababu. Na yote hayo yanaambatana na kutowajibishwa."
Aidha, Waziri wa Ulinzi wa Israel amesema makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano Gaza yanawezekana lakini akasisitiza kuwa suala la kumaliza vita ni jambo jingine.
Akizungumza na waandishi wa habari, waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant amesema kuwa kila kitu kimekamilika ili angalau kufikiwe makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda wa wiki sita pamoja na kuachiliwa kwa mateka wa Israel ambao bado wanashikiliwa na Hamas huko Gaza.
Soma pia: Borrell aeleza umuhimu wa "mamlaka imara ya Palestina" katika usalama wa Mashariki ya Kati
Gallant ambaye amesema kuwa makubaliano hayo ya muda yatawezesha kuleta hali ya utulivu eneo hilo ikiwa ni pamoja na eneo la kaskazini mwa nchi yake linalopakana na Lebanon, amesisitiza hata hivyo kwamba hayuko tayari kuvimaliza kabisa vita hivyo kama ilivyokuwa ikishinikizwa na Hamas, jambo ambalo limezusha maswali juu ya uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano hayo.
UN yalaani shambulio la Israel huko Khan Younis
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa na mratibu wa mchakato wa amani huko Mashariki ya Kati amelaani shambulizi la anga la Israel lililoendeshwa mapema leo katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya al-Mawasi huko Khan Younis, ambapo mamlaka za Gaza zinasema liliua watu 40.
Tor Wennesland, amesema sheria ya kimataifa ya kibinadamu ni lazima izingatiwe wakati wote huku akisisitiza kuwa raia kamwe wasitumiwe kama ngao katika mzozo huo. Hata hivyo Israel imekanusha idadi hiyo ya vifo na kusema mashambulizi yake yalikuwa yakiwalenga wanamgambo wa Hamas.
Mzozo huo ulianza Oktoba 7 mwaka jana baada ya wanamgambo wa Hamas kuvamia kusini mwa Israel na kuwaua watu 1,200 na kuwachukua mateka mamia ya wengine. Kulingana na wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel tayari yamesababisha vifo vya Wapalestina zaidi ya 41,000 huku wengine zaidi ya 94,000 wakijeruhiwa.
( Vyanzo: APE, DPAE, AP, Reuters)