Marekani yapitisha muswada wa kuiwekea vikwazo ICC
7 Juni 2024Muswada huo unaotoa uwezekano wa Mahakama ya ICC kuwekewa vikwazo umepitishwa kwa kura 247 dhidi ya 155 za wale walioupinga.
Kupitishwa kwake ni hatua ya kwanza ya bunge la Congress kuonesha kutoridhishwa kwake na hatua ya mahakama hiyo ya kimataifa kutaka waranti wa kukamatwa kwa viongozi wa Israel.
Hatua hii ya Bunge la Marekani imedhihirisha kwa mara kwanza mgawanyiko baina ya wanasiasa nchini humo kuhusu uungwaji mkono kwa Israel katika vita vyake dhidi ya kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Licha ya kuwa muswada huo ulitarajiwa kupitishwa katika Bunge hilo la Marekani lakini umewavutia wabunge wachache wa chama cha Democratic, jambo ambalo huenda likatatiza nafasi yake ya kupita katika Baraza la Senati. Hata Ikulu ya White House inaupinga muswada huo ikisema umechupa mipaka.
Je, muswada huo una nafasi gani kuwa sheria?
Wawakilishi wa vyama vya Republican na Democratic waliomo kwenye Kamati inayohusika na mambo ya nje katika Bunge hilo wamesema mswada huo una nafasi ndogo mno wa kuidhinishwa kuwa sheria na wakahimiza mazungumzo zaidi na Ikulu ya White House wakisema itakuwa bora kwa Baraza la Congress kuungana dhidi ya Mahakama hiyo ya ICC yenye makao yake mjini The Hague.
Soma pia: ICC na wafanyakazi wake walengwa na visa vya ujasusi
Mike McCaul, Mwenyekiti, Kamati hiyo ya Mambo ya Nje ya Bunge amesema:
"Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imevuka mamlaka yake na kuwacha historia ya hatari kwa kuomba vibali vya kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant, sambamba na magaidi wa Hamas. Ninataka kuwa muwazi: kesi dhidi ya Israel haina msingi."
Mswada huo unalenga kuwawekea vikwazo vya kiuchumi na sheria kali za maombi ya visa kwa watu binafsi, majaji na familia zao ambao watahibitika kuwa na mafungamano na ICC.
Hayo yakijiri, vita vinaendelea kurindima huko Gaza ambako Israel imeendeleza mashambulizi yake leo Jumatano na kusema sasa wameanzisha rasmi operesheni katikati mwa Gaza.
Wakati huo huo, timu ya wapatanishi kutoka Marekani, Misri na Qatar wanapanga kuanza tena mazungumzo yaliyokwama kuhusu makubaliano ya usitishwaji mapigano na kuachiliwa kwa mateka. Mzozo huu ulioanza Oktoba 7 mwaka jana baada ya shambulizi la Hamas kusini mwa Israel tayari limesababisha vifo vya Wapaletina zaidi ya 36,000, hii ikiwa ni kulingana na Wizara ya Afya inayodhibitiwa na Hamas ambayo imeorodheshwa na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na mataifa kadhaa ya Magharibi kama kundi la kigaidi.