1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

Hali ya utulivu yarejea katika jimbo la Amhara, Ethiopia

13 Aprili 2023

Hali ya utulivu imerejea katika jimbo la Amhara nchini Ethiopia, baada ya siku kadhaa za maandamano yaliyogeuka kuwa vurugu na kusababisha kuwekwa amri ya kutotoka nje kwa lengo la kuumaliza mzozo wa kiusalama.

https://p.dw.com/p/4Q0sw
Äthiopien | Augenoperationen für Menschen mit Grauem
Picha: Alemnew Mekonnen/DW

Mipango ya Serikali ya Shirikisho ya Ethiopia kutaka kuvijumuisha vikosi vya ulinzi vya  Amhara  katika jeshi na polisi la nchi hiyo, imesababisha maandamano ya siku kadhaa katika jimbo hilo la kaskazini, ambako taarifa zimeeleza kuwa watu kadhaa walipigwa risasi wakati wa maandamano yaliyofanyika siku ya Jumanne, ambayo ilikuwa ni siku ya sita mfululizo kuipinga mipango hiyo ya serikali.

Mkaazi mmoja wa mji wa Dessie, moja ya maeneo yaliyoshuhudia ghasia mbaya zaidi, ameiambia DW kwamba machafuko ya Jumanne yamepungua kwa kiasi kikubwa:

''Kulikuwa na matukio ya ufyatuaji risasi asubuhi, lakini nadhani ilikuwa kwa ajili ya kuwatawanya waandamanaji. Sasa hali imetulia, ingawa barabara bado zimefungwa.''

Wakati huo huo, matukio sawa na hayo yalishuhudiwa huko Bahir Dar, mji mkuu wa jimbo la Amhara. Mchambuzi huru wa  Ethiopia,  Alemnew Mekonnen ameiambia DW kwamba gadhabu iliyoshuhudiwa siku ya Jumanne imepungua, huku baadhi ya barabara kuu zikiendelea kufungwa:

''Sasa mambo yametulia. Jumanne kulikuwa na maandamano makubwa kwenye maeneo tofauti. Kulikuwa na fujo, lakini sasa kutoka pande zote, mambo yako katika hali ya kawaida.''

Alemnew anasema maisha yanaanza polepole kurejea katika hali ya kawaida kwa wakaazi baada ya wiki moja ya kutokuwa na utulivu, baadhi ya wafanyakazi wamerejea ofisini na huduma za usafiri zimeanza.

Äthiopien Bahir Dar | Friedlicher Protest gegen Premierminister Abiy
Maandamano ya amani dhidi ya Utawala wa Ethiopia huko BahirDar katika Jimbo la Amhara, 02.04.2023Picha: Alemenew Mekonnen/DW

Amri ya kutotoka nje iliwekwa katika miji mitatu mikubwa ya Gondar, Dessie na Debra Birhan, ili kuyadhibiti maandamano. Hatua hiyo ilifuatiwa na kukatwa kwa mtandao wa intaneti, hatua iliyochukuliwa na serikali ya Ethiopia kuuzima upinzani.

Soma pia: Watumishi wawili wa shirika la misaada ya Marekani wauawa, Amhara

Eshetu Getnet, mmoja wa walioshuhudia siku kadhaa za ghasia kati ya wanamgambo wa Amhara na Oromo katika maeneo jirani ya Ataye na Jile, ameiambia DW kwamba vikosi vya ulinzi vya serikali ya shirikisho vilisaidia sana kuleta utulivu. Eshetu anasema ni jambo la kupongezwa kwamba sasa vikosi vya ulinzi vinafanya kazi kwa haki.

Kutekeleza makubaliano ili kudumisha utulivu

Maafisa wa serikali ya shirikisho ya Ethiopia wamesema kuwa kukifuta Kikosi Maalum cha Amhara, ASF na makundi mengine ya wanamgambo kwenye majimbo 11 ya Ethiopia na kuvijumuisha katika jeshi la shirikisho au polisi, kutaunda kikosi chenye nguvu na umoja nchini humo, ambako migawanyiko imesababisha maelfu ya vifo katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Äthiopien Abiy Ahmed
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: Tiksa Negeri/REUTERS

Lakini waandamanaji wa Amhara wanasema kwamba mipango ya serikali italiacha jimbo lao katika hatari ya kushambuliwa na majimbo mengine. Hayo yanajiri baada ya ASF kuchukua jukumu muhimu sana katika vita vya serikali dhidi ya waasi wa Tigray, mzozo ambao umesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kuwaacha wengine wengi bila makaazi.

Soma pia: Vizuizi vyawekwa Amhara baadaya maandamano kupinga hatua ya serikali ya Ethiopia

Kukivunja na kukijumuisha katika jeshi la serikali kikosi cha ASF, ni sehemu ya mkataba wa amani na Tigray, masharti ambayo kwa sasa yanatekelezwa na serikali ya shirikisho. Alemnew Mekonnen ameiambia DW kwamba mamlaka inapaswa kujadiliana na watu, na vikosi maalum, na wadau wengine, ili kuwe na maelewano.

Blen Mamo Diriba, mtafiti wa Ethiopia katika Chuo Kikuu cha Birkbeck, London, Uingereza, ameiambia DW kwamba viongozi wa kijamii kutoka Amhara wanapaswa kimsingi kuushawishi umma kujizuia na kujiepusha na vitendo vya ghasia, akisisitiza kuwa kuutatua mzozo wa sasa jimboni Amhara ni muhimu katika kumaliza hali mbaya ya usalama kwa ujumla nchini Ethiopia.