Hayati Magufuli aagwa kwa majonzi makubwa Mwanza
24 Machi 2021Mwanza ni mkoa ambao Marehemu John Magufuli alipata kusoma na kufanya kazi na maelfu ya watu leo wamejitokeza barabarani kuanzia uwanja wa ndege wa Mwanza mpaka Uwanja wa michezo wa CCM Kirumba kwa ajili ya kumuaga marehemu Magufuli. Mwili huo uliwasili asubuhi katika uwanja wa ndege wa Mwanza ukitokea visiwani Zanzibar.
Vilio, kwikwi, watu kulala barabarani, kanga kutandikwa barabarani huku wengine wakiwa wameshika matawi ya miti pamoja na maua ndiyo ilikuwa taswira ya Mwanza katika kumlilia Marehemu John Magufuli, mwitikio ambao viongozi wa serikali na waombolezaji wote uliwasisimua.
"Niwashukuru sana wananchi wa mwanza, kama tutazungumza historia ya mzalendo huyu wa kweli wa taifa na mzalendo wa Afrika hayati raisi John Pombe Magufuli hatutaacha kuwakumbuka wana mwanza wana mchango mkubwa katika kukuza kipaji chake cha uongozi tunawashukuruni sana," alisema Jenista Mhagama ni Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu, sera uratibu na Bunge.
soma zaidi: Namna Rais Magufuli alivyoagwa Zanzibar
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewaongoza waombolezaji na akatoa neno la serikali kwa niaba ya rais Samia Suluhu Hassan.
"Mama yetu Samia Suluhu Hassan, anawapa salamu za pole wana kanda ya ziwa wote. Muheshimiwa raisi anawasihi katika kipindi hiki cha huzuni ya kuondokewa na mpwendwa wetu aliyekuwa rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli anaomba sana tuwe watulivu," alisema Waziri Mkuu wa taifa hilo la Afrika Mashariki.
soma zaidi: Matumaini ya Wazanzibari katika urais wa Samia Suluhu Hassan
Baada ya ya kutoka katika uwanja wa CCM kirumba mjini Mwanza, mwili wa Marehemu John Pombe Magufuli ulipitishwa katika maeneo mbali mbali ya ndani na nje ya mji huo ili kutoa fursa kwa watu mbali mbali kummpa mkono wa kwaheri hayati Magufuli.
Baadaye msafara huo utaelekea nyumbani kwake Chato mkoani Geita ambapo itakuwa sehemu ya mwisho ya safari yake atakapohifadhiwa katika nyumba yake ya milele.
Mwandishi: Dotto Bulendu DW Mwanza.