Hong Kong yazuia kumbukumbu ya Tiananmen
4 Juni 2021Polisi wapatao 7,000 waliomwagwa katika jiji la Hong Kong ilizuia njia za kuingilia bustani hiyo ya Victoria ambako makundi makubwa ya watu huwa yakikusanyika kwenye kuwakumbuka wahanga wa ukandamizaji uliofanywa na vikosi vya China na kusambaratisha maandamano ya amani katika uwanja wa Tiananmen nchini China Juni 4, 1989.
Baadhi wanakadiria kwamba zaidi ya waandamanaji 1,000 waliuawa kwenye tukio hilo.
Soma Zaidi: Maoni: Kimya kingi kisicho mshindo China
Shughuli ya umma kuhusiana na kumbukumbu ya kisa hicho imezuiwa China Bara na hadi hivi karibuni Hong Kong iliyo chini ya himaya ya China ilikuwa ni moja ya maeneo ambayo bado idadi kubwa ya watu walikuwa wanaendelea kuiadhimisha.
Kumbukumbu ya mwaka huu imezuiwa katika wakati ambapo mamlaka zinachukua hatua kali na pana dhidi ya wakosoaji kufuatia maandamano makubwa miaka miwili iliyopita na ambayo mara kwa mara yaligubikwa na vurugu. Hata hivyo mamlaka zinasema ni katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona, ambavyo hata hivyo hakujapatikana kisa kipya kwa zaidi ya mwezi sasa jijini Hong Kong.
Polisi waliweka vizuizi, ili kuwazuia watu kukusanyika kwenye bustani ya Victoria na kuliacha eneo hilo likiwa halina shamrashamra zilizozoeleka za watu kukusanyika wakiwa wamebeba mishumaa, ikiwa ni mara ya pili katika kipindi cha miaka 32.
Wanaharakati waliofika kwenye bustani hiyo walizuiwa na kupekuliwa, wakati maafisa wa polisi wakitumia vipaza sauti kuwatawanya waandamanaji waliokuwepo kwenye mitaa ya karibu. Wengine waliwaambia raia kwamba wanakiuka mageuzi ya sheria mpya ya usalama wa taifa, iliyoanzishwa na Beijing dhidi ya jiji hilo mwaka jana ili kuwazimisha wakosoaji.
Miongoni mwa wanafunzi waliojitokeza mapema leo na aliyejitambulisha kwa jina moja, Alberto alilalama alipozungumza na shirika la habari la AFP. "Ninahisi ni kama Hong Kong inazidi kukandamizwa lakini pia si mahali salama. Kuna ongezeko la polisi mitaani wanaowasimamisha watu na kuwapekua, ali mradi tu kuwachukulia hatua kali wakosoaji na kuwanyamazisha watu."
Hata hivyo bado watu wa Hong Kong wanatafuta namna nyingine za kuwakumbuka wahanga hao. Majira ya saa 8 usiku ambao kwa kawaida huwa wanawasha mishumaa, baadhi ya wakazi katika mitaa ya Causeway Bay na Mongkok waliwasha tochi za simu zao ya mkononi, hii ikiwa ni kulingana na mwandishi wa habari wa AFP. Wengine walitengeneza mishumaa na kuiwasha mahali walipokuwa na wengine walihudhuria ibada.
Soma Zaidi: Miaka 31 ya mauaji ya Tiananmen,maandamano yazuwiwa HongKong
China imekuwa ikikabiliwa na ukosoaji mkali kutokana na hatua zake kali, na mapema leo waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Anthony Blinken ametoa mwito wa kutolewa kwa idadi kamili ya waliouawa, kukamatwa na kupotea, na yenyewe kuijibu Marekani kwa kuiambia ijitazame kwenye kioo kuhusu rekodi yake ya haki za binaadamu.
Mashirika: AFPE/APE