1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICJ kuamua kuhusu mzozo wa mpaka kati ya Kenya na Somalia

Shisia Wasilwa12 Oktoba 2021

Mahakama ya Kimataifa ya Haki-ICJ itatoa uamuzi wake Jumanne kuhusu mzozo wa muda mrefu wa mpaka kati ya Kenya na Somalia.

https://p.dw.com/p/41Z17
Den Haag Internationaler Gerichtshof ICJ Entscheidung Bolivien Chile
Picha: Getty Images/AFP/J. Lampen

Kenya imepuuzilia mbali mamlaka ya mahakama hiyo kabla ya uamuzi huo, ikisema kuwa dhima yake ni ya kusuluhisha wala sio kutoa uamuzi. Mzozo huo, umeyumbisha mahusiano kati ya mataifa hayo jirani.

Somalia, ambayo inapakana na Kenya upande wa Kaskazini Mashariki, inataka kuongeza mpaka wake katika bahari hindi unaopakana kusini Mashariki mwa Kenya.

Soma pia: Nini chanzo cha uhasama kati ya Kenya na Somalia?

Kwa upande wake Kenya inataka mpaka huo unyooshwe upande wa mashariki, jambo ambalo litaongeza upana wake. Eneo hilo linalozozaniwa linasemekana kuwa na utajiri wa mafuta na gesi.

Mwezi Machi mwaka huu, Kenya iliahidi kususia kikao cha uamuzi huo ambao utafanyika siku ya Jumanne. Kama taifa linalojitawala, Kenya haitazingatia uamuzi wa mahakama ya kimataifa bila ya ruhusa yake, ilisema taarifa kutoka kwa Wizara ya mambo ya Nje iliyotumwa kwa vyombo vya habari.

Infografik Seegrenzen Somalia Kenia EN

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Somalia na Kenya mashakani

Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa uamuzi huo utakuwa msururu wa makosa katika mchakato wa kufanyika kwa haki.  Mahusiano kati ya Kenya na Somalia hajayajakuwa mazuri kutokana na masuala ya usalama na mpaka huo unaozozaniwa.

Eneo hilo la maji linalozozaniwa, ni kilomita mraba 100,000  sawa na maili 40,000 mraba. Kenya inashikilia kuwa imemiliki eneo hilo tangu mwaka 1979.

Mikutano miwili ilifanyika mwaka 2014 kutafuta mwarubaini juu ya mzozo huo, lakini hakuna hatua iliyopigwa. Awamu nyingine ya mkutano iliyofuatia mwaka huo ilifeli baada ya ujumbe wa Kenya kukosa kuhudhuria, bila kufahamisha upande wa Somalia.

Soma pia: Kenya na Somalia zakubaliana kutatua mzozo wao

Somalia iliwasilisha kesi hiyo mahakamani mwaka 2014, baada ya kudai kuwa majaribio ya kidiplomasia ya kuutatua mzozo huo uligonga mwamba.

Hata hivyo Kenya ambayo inaonekana kuwa msingi wa amani katika upembe wa Afrika inasisitiza kuwa imejitolea kutatua suala hilo.

Rais wa Somalia (Kushoto) pamoja na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.
Rais wa Somalia (Kushoto) pamoja na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

"Uamuzi ambao ICJ itatoa, ni maoni tu, hayana mashiko na kwa hivyo sio lazima Kenya  ikubaliane na maamuzi hayo," amesema Macharia Munene, mhadhiri wa masomo ya Historia na Mahusiano ya Kimataifa, katika chuo kikuu cha USIU nchini Kenya

Mabunge ya Taifa na Seneti nchini Kenya, tayari yameshamuomba Rais Kenyatta kuwatuma wanajeshi iwapo sehemu yoyote ya Kenya ikiwemo eneo linalozozaniwa na Somalia litakabiliwa na kitisho, tamko ambalo limekosolewa na Mahakama ya Kimataifa ya ICJ.

Uamuzi wa mahakama hiyo unasubiriwa kwa hamu na ghamu, haswa na Somalia ambayo ilikataa njia mbadala ya kutatua mzozo huo kupitia asasi za kidiplomasia za Umoja wa Afrika.
Uamuzi wa mahakama hiyo unasubiriwa kwa hamu na ghamu, haswa na Somalia ambayo ilikataa njia mbadala ya kutatua mzozo huo kupitia asasi za kidiplomasia za Umoja wa Afrika.Picha: Getty Images/AFP/B. Czerwinski

"Mahakama ya ICJ ni mahakama ya kusuluhisha, sio mahakama ambapo haki hutekelezwa. Huwezi kusuluhisha mzozo wa majirani wawili ambao hawajazungumza. Unasuluhisha nini? Somalia haijawahi kupinga eneo hilo kuwa la Kenya, ili kuingilia himaya ya Kenya kwa kipindi kirefu,” amesema Peter Kwagwanja.

Mwaka 2019 Kenya ilimuita nyumbani balozi wake kutoka Mogadishu kwa tuhuma za kuuza mafuta na gesi katika eneo linalozozaniwa.

Hata hivyo mataifa hayo yalikubaliana kurejesha mahusiano yao baada ya Waziri Mkuu wa Somalia Mohamed Hussein Roble kufanya mazungumzo na Rais Kenyatta Agosti mwaka huu.